Wahitimu: Mafunzo Veta pekee si suluhisho la ajira

Simiyu. Baadhi ya wahitimu wa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (Veta) wamesema, licha ya kupata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kufanya kazi mbalimbali, bado mafunzo hayo peke yake hayatoshi kutatua changamoto ya ajira.

Badala yake wameshauri kuwepo mazingira rafiki ya kukuza sekta binafsi na upatikanaji wa mitaji.

Wakizungumza na Mwananchi Digital Machi 28, 2026, wahitimu hao wamesema ili ujuzi wanaoupata uweze kuleta tija, ni muhimu Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kukuza sekta binafsi pamoja na kuwezesha vijana kupata mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Mhitimu wa kozi ya umeme katika Chuo cha Veta Mwanza, Emmanuel Joseph amesema licha ya kuhitimu mwaka jana na kupata ujuzi mzuri wa vitendo, bado hajapata ajira ya kudumu.

“Tumepata ujuzi mzuri, lakini changamoto kubwa ni mtaji. Bila mtaji ni vigumu kufungua karakana au kununua vifaa vya kazi, hivyo wengi wetu tunabaki nyumbani,” amesema.

Kwa upande wake, mhitimu wa kozi ya ushonaji katika Chuo cha Ufundi Stadi Binza, Maswa, Chiku Hassan amesema vijana wengi wanashindwa kujiajiri licha ya kuwa na ujuzi kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuanzia kazi.

“Serikali inahamasisha vijana tujiajiri, lakini mashine za kushona na vifaa vingine ni ghali. Mikopo nafuu kwa wahitimu wa Veta ingeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney (aliye na skafu) akipata maelezo kutoka kwa vijana wanaosoma mafunzo ya ufundi bomba katika chuo cha  ufundi na maendeleo ya wananchi Malampaka wilayani humo. Picha na Samwel Mwanga

Naye John Paul amesema ukuaji mdogo wa sekta binafsi unachangia uhaba wa ajira kwa wahitimu wa vyuo vya ufundi, akieleza kuwa ingawa wahitimu wanaongezeka kila mwaka, idadi ya viwanda na karakana kubwa zinazoweza kuwaajiri bado ni ndogo.

“Sekta binafsi ikipewa mazingira bora ya kufanya biashara, itaweza kuajiri vijana wengi zaidi,” amesema.

Akizungumzia suala hilo, mchumi Jerry Nyabululu amesema mafunzo ya ufundi ni hatua muhimu katika kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi, lakini hayatoshi peke yake kutatua tatizo la ajira.

“Ajira nyingi duniani zinatokana na sekta binafsi. Bila ukuaji wa kasi wa sekta hiyo, hata ongezeko la wahitimu wa Veta halitaondoa changamoto ya ajira,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sera rafiki zinazowezesha uwekezaji katika viwanda vidogo na vya kati, ambavyo vina uwezo mkubwa wa kuajiri wahitimu wa vyuo vya ufundi.

Kwa upande wake, mtaalamu wa masuala ya ajira na maendeleo ya vijana, Peter Maingu amesema ukosefu wa mitaji na mifumo madhubuti ya kuwaunganisha wahitimu na fursa za ajira ni miongoni mwa changamoto kuu zinazowakabili vijana wengi.

“Ni muhimu kuwepo kwa mifumo ya mikopo midogo midogo pamoja na kuwajengea uwezo wa uendeshaji wa biashara. Bila hatua hizo, ujuzi walioupata unaweza usiwe na tija,” amesema.

Ameongeza kuwa pamoja na kuimarisha mafunzo ya ufundi, Serikali na wadau wanapaswa kuwekeza zaidi katika kukuza uchumi wa viwanda na biashara ndogo ndogo ili kuongeza ajira kwa vijana.

Amesema endapo juhudi za kukuza sekta binafsi zitaenda sambamba na mafunzo ya ufundi, wahitimu wa Veta wataweza kutumia ujuzi wao kikamilifu na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya uchumi wa taifa.