Dosari za kisheria zamnusuru aliyekuwa askari

Arusha. Mahakama ya Rufani nchini imebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu ulioamuru kusikilizwa upya kwa kesi ya ulawiti iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa askari mwenye cheo cha Sajenti (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili), aliyeshtakiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto wake wa kumzaa aliyekuwa na umri wa miaka saba.

Mahakama imebatilisha uamuzi huo baada ya kubaini kuwepo kwa kasoro kubwa za kisheria katika kesi hiyo.

Awali, askari huyo alifikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Singida akikabiliwa na shtaka la ulawiti kinyume na kifungu cha 154 (1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba 2021 na mwaka 2023.

Mahakama hiyo ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha maisha jela, na kutokana na kutoridhika na adhabu hiyo alikata rufaa ya kwanza Mahakama Kuu, ambayo ilibatilisha hukumu hiyo na kuamuru kesi kusikilizwa upya badala ya kuachiliwa huru mrufani.

Uamuzi uliomwachia huru mrufani huo umetolewa Machi 27, 2026, na jopo la majaji watatu ambao ni Zephrine Galeba, Dk Benhajj Shabaan Masoud na Dk Eliezer Feleshi, waliokuwa wakisikiliza rufaa ya jinai namba 745523/2024.

Jaji Galeba amesema baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa, Mahakama imejiridhisha kuwa dosari za kisheria zilizojitokeza wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo hadi uamuzi wake, zimefanya kesi nzima kuwa batili, hivyo kuamuru mrufani aachiliwe huru.

Awali, katika Mahakama ya Wilaya, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi nane, ambapo ilidaiwa mrufani katika eneo la Polisi la Utemini mkoani Singida alikuwa akitenda kosa hilo kwa kipindi hicho.

Katika rufaa ya kwanza (Mahakama Kuu), Mahakama iliruhusu rufaa hiyo kwa kiasi fulani, ambapo ilibatilisha hukumu hiyo baada ya kubaini kuwa baadhi ya ushahidi wa mashahidi haukusainiwa na Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo na kuamuru kesi hiyo ikasikilizwe upya.

Katika rufaa ya pili, mrufani alikuwa akiwakilishwa na wakili mmoja huku mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili watatu.

Wakili wa mrufani alidai kuwa kulikuwa na makosa makubwa mawili yaliyoathiri haki ya mteja wake, ambapo alidai kuwa hati ya mashtaka ilirekebishwa mara kadhaa, lakini mrufani alihukumiwa kwa kutumia shtaka la awali.

Alidai hati ya shtaka ya awali ilikuwa inaonesha kuwa kosa aliloshtakiwa lilitendeka kati ya Oktoba 2021 hadi Machi 18, 2023, huku hati iliyorekebishwa ikionesha kosa kufanyika Aprili 12, 2023, na baadaye tena likioneshwa kufanyika Oktoba 2021 hadi Desemba 2022.

Wakili huyo alidai hati ya mwisho iliyorekebishwa ilipunguza muda huo hadi Desemba 2022, hata hivyo, mahakama za chini ziliendelea kurejea shtaka la awali katika hukumu zao.

Pili, wakili huyo alieleza kuwa sehemu kubwa ya ushahidi wa mashahidi haukusainiwa na hakimu wa kesi, jambo linaloathiri uhalali wa ushahidi huo kisheria.

Kwa upande wa Jamhuri, ilikiri kuwepo kwa dosari hizo, lakini ilisisitiza kuwa hazikusababisha madhara makubwa kwa mrufani, na ikaomba mahakama iamuru kesi hiyo irudiwe ili haki ipatikane kwa pande zote.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani haikukubaliana na hoja hiyo ya upande wa mashtaka, ambapo katika uchambuzi wake wa kina, mahakama ilieleza kuwa msingi wa kesi yoyote ya jinai ni hati halali ya mashtaka, na pale ambapo shtaka hilo lina kasoro kubwa, basi kesi nzima hupoteza uhalali wake.

Mahakama ilibaini kuwa baada ya shtaka kurekebishwa, shtaka la awali lilipaswa kufutwa na lisitumike tena katika hatua yoyote ya kesi.

Jaji Galeba amesema ushahidi na hukumu za mahakama za chini zilionesha wazi kuwa kesi iliendeshwa kwa kuzingatia shtaka ambalo halikuwa halali tena.

Aidha, majaji walieleza kuwa kuamuru kesi kusikilizwa upya kungekuwa sawa na kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka kurekebisha makosa yao, jambo ambalo si sahihi kisheria na linaweza kuathiri haki ya mshtakiwa.

Mahakama imesisitiza kuwa haki ya mshtakiwa ni msingi muhimu katika mfumo wa haki za jinai, na kwamba makosa ya msingi katika mwenendo wa kesi hayawezi kurekebishwa kwa kuanzisha upya shauri, hasa pale ambapo dosari hizo zinatokana na uzembe au ukiukwaji wa taratibu za kisheria.

Kutokana na hoja hizo, Mahakama ya Rufani imefikia hitimisho kwamba kesi dhidi ya mrufani ilikuwa batili tangu mwanzo, na hivyo haikuwa sahihi kuendelea nayo kwa namna yoyote ile.

Kwa kutumia mamlaka yake ya kisheria, mahakama imebatilisha amri ya Mahakama Kuu iliyotaka kesi hiyo irudiwe, na badala yake ikaamuru mrufani aachiwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.

“Kwa kuzingatia mamlaka ya Mahakama hii chini ya kifungu cha 6 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, tunaweka kando agizo la kusikilizwa upya kwa kesi kama ilivyoamriwa na Mahakama ya kwanza ya Rufaa.

“Amri ya kuwasilisha rekodi mahakama ya chini kwa ajili ya kurekebisha hukumu pia inakataliwa, na badala yake tunaamuru kwamba mrufani aachiliwe huru kutoka gerezani isipokuwa kwa sababu nyingine yoyote halali,” imehitimisha hukumu hiyo