Arusha. Zikiwa zimepita siku 33 tangu agizo la Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, la kurejeshwa kwa mali za mfanyabiashara wa Arusha, Josephine Shirima, mali hizo bado hazijarudishwa na sasa suala hilo linashughulikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Februari 24, 2026, mbele ya Waziri Mkuu, Josephine alidai kuwa Makoi pamoja na Mollel walihusika kumdhulumu mali zake zilizokuwa dukani.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumamosi, Machi 28, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema kwa sasa suala hilo limeshatoka kwenye ngazi yake na ya mkoa na linashughulikiwa na ofisi hiyo.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo inashughulikia, suala limeshatoka kwangu na kwa ngazi ya mkoa. Sisi tulishafikia ukomo wetu wa kutekeleza, tumetekeleza, sasa lipo kwenye hatua nyingine kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu,” amesema Mkude.
Awali, Machi 12, 2026, Mkude alisema walikuwa wakimshikilia dalali wa Mahakama (jina halikutajwa), huku Molle akiachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea.
“Tunamshikilia dalali wa Mahakama na tunaendelea kuwatafuta wengine wanaodaiwa kushirikiana naye katika suala hilo,” alieleza Mkude.
Amesema lengo kuu ni kuhakikisha mali za mfanyabiashara huyo zinapatikana, licha ya mgogoro huo kudumu zaidi ya miaka minne.
Awali, Februari 24, 2026, Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Josephine kudai katika mkutano wa hadhara jijini Arusha kuwa duka lake lilivunjwa usiku na mali zake kuchukuliwa. Waziri Mkuu alimuagiza Mkude kuhakikisha mali hizo zinarejeshwa haraka kabla ya hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa Josephine, mgogoro huo unatokana na maduka ya stendi ndogo ya Arusha yaliyokuwa yamejengwa kwa mkataba wa miaka 10, ambapo baada ya mkataba kuisha walipaswa kuyarejesha kwa halmashauri, lakini baadhi ya watu waliendelea kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Mollel alidai Josephine alikuwa mpangaji ambaye hakuwa analipa kodi, na walifuata utaratibu wa kuwachukulia hatua wapangaji waliokuwa wanadaiwa, kwa ushirikiano na askari pamoja na dalali wa Mahakama.
Hata hivyo, viongozi wa Serikali walisisitiza kuwa mali hizo zilichukuliwa bila kufuata taratibu za kisheria, na uchunguzi utaendelea huku jitihada za kuzitafuta mali hizo zikiendelea.
