Arusha. Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masijala Ndogo ya Songea, imewaachia huru washtakiwa sita, akiwemo baba na wanawe wawili waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za ugaidi, baada ya kubaini kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka haukutosha kuthibitisha hatia yao.
Walioachiwa huru katika kesi hiyo ni Sefu Abdallah, Abdallah Mbwana, Mohamed Sadiki, Athumani Abdallah, Omari Hussein, na Rashid Bilahi.
Uamuzi wa kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao sita umetolewa Machi 24, 2026 na Jaji Athumani Matuma, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi.
Washtakiwa wote sita walikuwa wameshtakiwa kwa makosa mawili, ambapo kosa la kwanza ni kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi kinyume na kifungu cha 4 (1), 2 (b)(iii) na 27 (c) cha Sheria namba 21/2002 ya Kuzuia Ugaidi, ikisomwa pamoja na aya ya 24 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Kupangwa, Sura ya 200 (EOCCA). Shtaka la pili lilikuwa kushiriki katika mikutano ya ugaidi.
Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi wanne, ambapo watatu kati ya mashahidi hao walidai kurekodi maelezo ya onyo ya washtakiwa hao.
Shahidi wa kwanza alieleza kuwa Machi 3, 2020, akiwa na maofisa wengine 10, waliitwa na kiongozi wao na kuarifiwa kuhusu taarifa za vitendo vya kigaidi ndani ya mkoa wa Ruvuma, Mtwara, na nchi jirani ya Msumbiji.
Alidai kuwa walisafiri hadi Kijiji cha Lukumbule, wilayani Tunduru, kwa nia ya kuimarisha usalama, kwani kijiji hicho kipo mpakani, na Julai 13, 2020 walijulishwa kuwa kuna watu wanashiriki kupanga vitendo vya kigaidi.
Alidai kuwa walifanya maandalizi ya kuwakamata washukiwa hao ambapo walifanikiwa kumkamata mshtakiwa wa tatu, kisha wakaenda nyumba nyingine na kuwakamata washukiwa watatu ambao ni baba na wanawe wawili (mshtakiwa wa kwanza akiwa baba, wa pili na wa nne wakawa wanawe). Baadaye walifika saa mbili asubuhi Kituo cha Polisi Tuduma na kukabidhiwa washtakiwa hao.
Kumbukumbu za mahakama zinaonesha kuwa mashahidi watatu walidai kurekodi maelezo ya onyo ya washtakiwa hao na kuwa walikiri kushiriki katika vitendo vya kigaidi na kueleza kwa kina jinsi kila mshtakiwa alivyokuwa amejipanga kujiunga na makundi ya kigaidi nje ya nchi (Msumbiji) kwa lengo la kupata mafunzo ya kijeshi ili warudi nchini kupigana na Serikali na kuanzisha dola ya kiislamu.
Hata hivyo, washtakiwa wote walikana tuhuma hizo na kudai kuwa hawakuwahi kutoa kauli za kukiri wala kushiriki katika vitendo hivyo na kuwa walikamatwa katika kijiji cha Lukumbule, wilayani Tunduru, na kushikiliwa hadi walipofikishwa mahakamani bila kupelekwa Mtwara kama ilivyodaiwa na upande wa mashtaka.
Katika uchambuzi wake, Mahakama ilieleza kuwa msingi mkubwa wa kesi ya upande wa mashtaka ulikuwa ni maelezo ya onyo (maungamo) ya washtakiwa, ambayo hata hivyo yalipatikana kwa kukiuka taratibu za kisheria na hivyo kupunguza uzito wake wa kuthibitisha makosa.
Mahakama ilibaini mapungufu makubwa katika namna ushahidi huo ulivyopatikana na kuwasilishwa, ikiwemo kuchelewa kurekodi kauli za washtakiwa na kukosekana kwa maelezo muhimu ya kisheria kuhusu mazingira ya mahojiano.
Jaji amesema kulikuwa na mashaka makubwa juu ya uaminifu wa mashahidi wa upande wa mashtaka, hususan maofisa wa polisi waliorekodi taarifa hizo.
Mahakama pia ilibaini kwamba baadhi ya mashahidi walitoa ushahidi unaokinzana na taarifa zao za awali, huku wengine wakishindwa kueleza kwa usahihi taratibu walizofuata katika kurekodi kauli za washtakiwa.
Aidha, kulikuwa na migongano ya maelezo ndani ya kauli za washtakiwa wenyewe, hali iliyoashiria kuwa taarifa hizo hazikuwa maungamo ya kweli na haziwezi kutegemewa kisheria kuthibitisha hatia.
Katika uchambuzi wake, Mahakama ilisisitiza kuwa hata pale ushahidi unapokubaliwa licha ya kupatikana kinyume cha sheria, ni lazima uthibitike kuwa wa kuaminika, wa hiari, na wenye ukweli usio na shaka, jambo ambalo halikuthibitika katika kesi hiyo.
Mahakama pia ilikosoa utegemezi mkubwa wa upande wa mashtaka kwenye maelezo ya onyo bila kufanya uchunguzi wa kina kupata ushahidi huru wa kuunga mkono madai yao, ikisisitiza kuwa maelezo ya onyo pekee hayatoshi kuthibitisha kosa bila kuwepo kwa ushahidi mwingine thabiti.
Kutokana na upungufu huo, Mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi yao bila kuacha shaka yoyote.
“Baada ya kupitia hoja hizo, hakuna ushahidi wowote kuthibitisha hatia ya washtakiwa katika madai wanayoshtakiwa; kwa hiyo naona washtakiwa wote sita hawana hatia katika mashtaka yote mawili. Naamuru waachiliwe huru kutoka kizuizini isipokuwa kama wameshikiliwa kwa sababu nyingine halali. Haki ya kukata rufaa imeelezwa kwa yeyote ambaye hajaridhika na hukumu hii,” amehitimisha Jaji.
