Mchezo wa Kabaddi ulivyo na namna unavyochezwa

INAWEZEKANA ulishawahi kusikia mchezo unaoitwa Kabaddi na unatamani kujua kiundani mchezo huo namna unavyochezwa au unaona unavyoochezwa lakini huelewi. Lakini unatakiwa ufahamu kwamba, ili kukusanya pointi, huko inabidi kazi kubwa ifanyike.

Kabla ya kwenda mbali, unatakiwa ufahamu kwamba, Kabaddi ni mchezo wa kale wenye asili ya India, uliotokana na mazoezi ya kivita na mbinu za kujihami, ukikadiriwa kuwepo kwa zaidi ya miaka 4,000.

Mchezo huo unaaminika kwa kuchochewa na hadithi za kishujaa za Abhimanyu kutoka kwenye andiko la Mahabharata, likiwa na lengo la kuimarisha nguvu, pumzi na uwezo wa kukabiliana na maadui wengi kwa wakati mmoja.

Mwaka 2004, lilianzishwa Shirikisho la Kimataifa la Kabaddi (IKF) ili kusimamia mchezo huo ambao kwasasa umeenea duniani kote.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Kabaddi Zanzibar, Ramadhan Mrisho, ametoa elimu juu ya mchezo huo akisema kwa kawaida unakusanya jumla ya wachezaji 14 wa timu moja, kati yao wachezaji saba wanaanza na wengine saba wanasubiri nje.

Alisema, mchezo huo unaochezwa kwa kutumia timu Zoni A na B, huchezwa kwa dakika 40 zilizogawanywa kwa vipindi viwili kila kimoja kina dakika 20.

“Pointi kwenye mchezo huu zinapatikana baada ya mchezaji mmoja kutoka kwa timu ya Zoni A kwenda kufanya mashambulizi kwa wachezaji saba waliopo kwenye Zoni B.

“Kwa maana hiyo, wachezaji saba kutoka kwa timu Zoni B wanakuwa walinzi (defender) na mchezaji mmoja kutoka kwa timu ya Zoni A anakuwa mvamizi (rider).

“Rider anapoingia kwenye Zoni ya defenders anatakiwa atamke neno Kabaddi kwa sekunde 30 huku akipambana ili asikamatwe na wachezaji saba wasiguswe,” alisema.

Alifafanua kuwa, pointi za mchezo huo zinapatikana kwa mifumo miwili ikiwemo kuwagusa wachezaji saba (kwa kugusa kuanzia mmoja na kuendelea) na baada ya kuwagusa anatakiwa kuwahi mstari wa kati (middle line), hapo ndipo zinazopatikana.

Katika hatua nyingine, endapo mvamizi atawagusa wachezaji saba na kufanikiwa kudhibitishwa asifike kwenye mstari wa katikati, inahesabika hana pointi kwa sababu hajavuka kikwazo cha watu saba.

Pia, mfumo mwingine wa upatikanaji wa pointi endapo mvamizi ataingia kwenye mstari wa hatari wa Zoni B na kuwagusa bila ya wapinzani kumdhuru, hao walioguswa wanatakiwa kutoka nje ya uwanja na hapo atakuwa amevuna alama ya ziada (bonus point).

“Kwahivyo, mvamizi ili akamilike kupata kwake pointi kamili anapaswa kuwagusa walinzi wote saba na kuufikia mstari wa katikati, ndipo anapata pointi kamili, mbali na hapo hakuna kitu,” alisema.