Magata atwishwa zigo Mtibwa Sugar

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mkenya Yusuf Chippo, amesema kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Fredrick Magata, ndiye chaguo lake la kwanza kikosini hapo katika upigaji wa penalti msimu huu, labda ikitokea mchezaji huyo ana changamoto yoyote.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chippo alisema sababu za kumchagua mchezaji huyo ni kutokana na kazi nzuri anayoifanya akiwa mazoezini, licha ya baadhi ya nyota wenzake pia kuonyesha ubora unaofanana, japo tofauti ni utayari wa kila mmoja wao.

“Wapo wachezaji wazoefu ambao wangeweza kupiga, lakini ukiangalia utayari wake na jinsi anavyofanya akiwa mazoezini hata ungekuwa sehemu ya benchi la ufundi ungempa majukumu hayo, kinachombeba zaidi ni ile hali ya kujiamini,” alisema Chippo.

Akizungumzia suala hilo, Magata alisema majukumu yoyote atakayopewa na benchi la ufundi atayafanya kwa ustadi wa hali ya juu kwa ajili ya timu hiyo, ingawa moja ya jambo kubwa na la muhimu ili kufikia mafanikio ni kuendeleza mshikamano.

Katika penalti mbili za Mtibwa Sugar msimu huu katika Ligi Kuu Bara, amepiga Magata na kufunga zote, akiendelea kuaminiwa ambapo nyota huyo ndiye anayeongoza kwa mabao kwenye kikosi hicho akiwa amefunga matatu, sawa na Ismail Mhesa.

Miongoni mwa vitu vya kuvutiwa kwake ni mchezaji anayeshikilia rekodi ya kupandisha timu mbili kwenda Ligi Kuu kutokea Ligi ya Championship baada ya kuanza akiwa na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022 kisha Mtibwa Sugar msimu wa 2024-2025. Msimu wa 2024-2025 Magata alichangia mabao 30 ya Mtibwa kati ya 58, baada ya kufunga tisa na kuasisti 21, ambapo timu hiyo ilimaliza mabingwa na pointi 71, ikiungana na Mbeya City kurejea Ligi Kuu iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 68.