Akili Unde kuimarisha kilimo, mifugo Zanzibar

Unguja. Taasisi ya Teknolojia ya India Madras Kampasi ya Zanzibar (IITMZ) imedhamiria kuendeleza ushirikiano na taasisi mbalimbali za kitaaluma na kitafiti ndani na nje ya nchi kwa maendeleo ya elimu, utafiti na ubunifu kiteknolojia.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Dhamana (Mkuu) wa IITMZ, Profesa Prabhu Rajagopal wakati wa ziara ya siku moja ya watendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar (Zaliri) waliofika katika Kampasi ya IITMZ Bweleo, kwa lengo la kujenga uhusiano na kujifunza baina ya taasisi hizo mbili.

Katika mazungumzo hayo leo Machi 28, 2026, Profesa Rajagopal amesema IITMZ ni taasisi inayoongoza nchini India katika elimu ya teknolojia, hivyo kwa kushirikia na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inalenga kuleta elimu bora na ya juu ya masuala ya kiteknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Ina wajibu wa kuendesha ufundishaji, utafiti na ubunifu wa kiteknolojia unaozingatia mahitaji ya ndani huku ikiwa na ushindani wa kimataifa,” amesema.

Katika mazungumzo hayo, Msaidizi Mkuu Masuala ya Taaluma wa IITMZ, Profesa Suresh Akkihebbal ameithibitishia Zaliri kuwa IITMZ inatagemea kuwa na mchango mkubwa kiteknolojia na kitafiti katika harakati za masuala ya sekta ya kilimo yanayoendeshwa na taasisi hiyo.

Kadhalika, ameonyesha umuhimu wa IITMZ kuzitambua moja kwa moja jamii ambazo Zaliri inazifanyia kazi.

Mtafiti wa Mifugo wa Zaliri, Dk Othman Juma Othman amesema wamepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika kuimarisha maabara zake, ambazo zimeundwa kuwa za kisasa zaidi kwa uendeshaji wa shughuli na vipimo na tafiti Unguja na Pemba.

“Hivyo, kuna uhitaji mkubwa wa utumiaji wa teknolojia ya Akili Unde (AI) ambayo inaweza kutolewa kupitia kwa wataalamu kutoka IITMZ,” amesema.

Mwanafunzi wa shahada ya pili katika fani ya Sayansi ya Data na Akili Unde anayesomea katika Kampasi za IITMZ, Patrick Ndowo ametumia fursa hiyo kutoa wasilisho lake lililohusu utaalamu wa upimaji wa zao la karafuu lililobeba jina Clove Grading AI Project.

Wasilisho hilo linalenga katika uimarishaji wa njia bora zaidi ya utambuaji wa ubora wa karafuu kwa kuangazia viwango vya zao hilo, madaraja kuelekea kukuza soko la Taifa na kipato cha mkulima.

Ziara ya ujumbe wa Zaliri Kampasi ya IITMZ ni hatua ya kwanza yenye tija kuelekea ushirikiano wa utafiti unaolenga kuleta maendeleo kwa sekta ya kilimo na ufugaji Zanzibar na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Mazungumzo hayo yenye maana kuhusu kazi za taasisi hizo mbili na ulinganifu wao ni dhahiri yataleta ujuzi wa kina wa kilimo na ufugaji huku maabara ya IITMZ inatagemewa kuchangia uwezo wa sayansi ya data na akili unde iliyobuniwa mahsusi kwa muktadha wa Kiafrika.