Wavuvi watakiwa kuzingatia tahadhari za hali ya hewa

Tanga. Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Bahari ya Hindi mkoani Tanga wametakiwa kuzingatia na kufuata taarifa za hali ya hewa, ili kujiepusha na ajali zinazoweza kusababisha vifo kutokana na mabadiliko ya yanayotokea.

Wito huo umetolewa na mkaguzi wa vyombo vya majini kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania  (Tasac) Mkoa wa Tanga, Seleman Pazzy, wakati wa utoaji wa elimu ya usalama wa majini na matumizi sahihi ya vyombo vya usafiri katika Bahari ya Hindi.

Amesema kutofuata utabiri wa hali ya hewa kumeendelea kuwa chanzo kikuu cha ajali nyingi za majini, akitolea mfano ajali iliyosababisha vifo vya watu watano waliokuwa wakisafiri kutoka Pangani kwenda Mkokotoni, Unguja, iliyochangiwa na kupuuza tahadhari za hali ya hewa.

Sambamba na hilo, imebainika kuwa wavuvi wengi katika mwambao wa Wilaya ya Mkinga hawana utamaduni wa kuvaa majaketi ya uokozi wanapokwenda baharini, hali inayoongeza hatari ya kupoteza maisha pindi ajali zinapotokea.

Uchunguzi uliofanywa katika maeneo ya Mwalo wa Petukiza, Mwaboza na Moa umeonyesha kuwa wavuvi wengi huingia baharini bila kutumia vifaa hivyo muhimu vya usalama.

Hali hiyo pia imeonekana katika baadhi ya vyombo vinavyomilikiwa na vikundi au miradi ya maendeleo ambavyo, licha ya kupewa majaketi, hayatumiki ipasavyo.

Sababu zinazochangia hali hiyo ni pamoja na ukosefu wa elimu ya usalama wa majini, gharama za ununuzi wa majaketi pamoja na mtazamo hasi miongoni mwa baadhi ya wavuvi wanaodhani kuwa kuvaa jaketi si jambo la lazima.

Kwa mujibu wa sheria za usafiri wa majini, matumizi ya vifaa vya uokozi ni ya lazima, na vyombo vinavyokiuka vinaweza kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini au kuzuiwa kufanya kazi.

Msimamizi wa boti katika eneo hilo, Hassan Wembe, amesema elimu inayotolewa ni muhimu lakini bado uelewa ni mdogo miongoni mwa wavuvi wengi.

“Elimu hii ni muhimu kwa wadau wa bahari, lakini bado wavuvi wengi hawaoni ulazima wa kuvaa majaketi. Hata hivyo, jaketi hupunguza madhara kwa kiasi kikubwa pale ajali inapotokea,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Wasimamizi wa Rasilimali za Bahari (BMU) Zingibari, Juma Hassan amesema baadhi ya wamiliki wa vyombo hawana utamaduni wa kuwapatia wavuvi vifaa vya uokozi, na ameiomba TASAC kuendelea kusimamia sheria na kutoa elimu ili kuhakikisha vyombo vinazingatia matakwa ya usalama.

Kwa upande wake, mmiliki wa boti Abdallah Issa amesema changamoto kubwa ni kipato kidogo kinachowakwamisha kununua vifaa hivyo, licha ya umuhimu wake katika kuokoa maisha, hususan kwa watu wasiojua kuogelea.

Viongozi wa maeneo hayo wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuongeza elimu kwa wavuvi ili kubadili mtazamo wao kuhusu usalama wa majini.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Moe, Massa Khalid, amesema ni muhimu pia kwa vyombo vyote vya majini kuwa na mifumo ya mawasiliano kwa ajili ya kupokea tahadhari za dharura.

Kwa ujumla, wadau wanakiri kuwa changamoto za kipato na uelewa bado zinachangia baadhi ya wavuvi kupuuza matumizi ya majaketi ya uokozi.

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa kuzingatia taarifa za hali ya hewa na kutumia vifaa vya usalama ni hatua muhimu katika kuokoa maisha ya wavuvi baharini.