Wadau wafunguka kifo cha mfanyabiashara aliyesombwa na maji na familia yake

Dodoma/Dar. Kifo cha mfanyabiashara na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, Yusuph Mwandami na familia yake, kimeibua hisia za wengi, wakimkumbuka kwa matendo yake enzi za uhai wake.

Mwandami, alifariki dunia Machi 26, 2026 saa 1:00 usiku katika Kata ya Mang’onyi mkoani Singida, baada ya gari walilokuwa wakisafiria na familia yake kusombwa na maji na wote waliokuwemo yeye, mkewe, mwanawe na dereva wamepoteza maisha.

Taarifa za vifo hivyo ziliripotiwa Ijumaa Machi 27, 2026 usiku baada ya kusambaa katika mitandao ya kijamii na baadaye kuthibitishwa Polisi na ndugu wa karibu.

Hadi Jumamosi jioni, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida lilikuwa limeopoa miili ya watu wawili, Yusuph na mkewe huku juhudi za kutafuta miili ya dereva na mtoto aliyetambulika kwa jina la Sabri zilikuwa zikiendelea.

Kaimu Kamanda wa Zimamoto, Devotha Bigawa, alisema mbali na mwili wa Mwandami uliokutwa kwenye mashamba ya mpunga Bahi, mwili mwingine waliofanikiwa kuuopoa ulikuwa wa Luluwa Selemani ambaye ni mke wa marehemu.

Akizungumzia tukio hilo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Singida, Martine Lissu, amesema jana (Machi 27) alianza kupokea taarifa ya mvua kubwa iliyonyesha katika Mkoa wa Singida.

Taarifa ya mvua, amesema iliambatana na tukio la kuzama kwa Mwandami, aliyekuwa na mkewe na mwanawe, wakitoka kwenye shughuli zao za kila siku kurudi nyumbani kwao.

Kwa taarifa alizopokea, Lissu amesema aliambiwa Mwandami akiwa na familia yake kutoka kwenye shughuli za kila siku kurudi nyumbani, walikuta daraja moja limejaa maji kiasi kwamba halionekani.

Amesema wote watatu wakiwa na dereva wa gari walilokuwa wanatumia walishuka kwenye gari kuangalia wingi wa maji na wakakubaliana kwamba kuna uwezekano wa kupita.

“Kwa nilivyoambiwa mkewe alikataa kupanda gari, akamtania kwamba usipopanda mimi na wewe basi, lakini kwa utani. Wakakubaliana kupanda gari wakaanza kuvuka daraja,” amesimulia.

Amesema walianza kuvuka daraja, wakiwa katikati tairi moja likatoka darajani na kuingia korongoroni, dereva akataka kurudisha gari nyuma, daraja likamomonyoka zaidi.

“Kuanzia pale Mwandami akawa anahangaika kufungua mlango, lakini maji yalimzidi nguvu hatimaye wakazama wote,” amesema.

Amesema mkewe ndiye aliyekuwa wa kwanza kupatikana na baadaye jioni yeye mwenyewe alipatikana katika Kijiji cha Nsemembo katikati ya Manyoni na Ikungi.

Katika hatua nyingine, Martine Lissu alisema asili ya marehemu ni Mwanza, lakini aliishi sana Singida na ndiye aliyeisaidia timu ya Singida United kujiendesha, pale ilipoonekana imekufa.

Amesema alifanya kila juhudi kuifanya Singida United iinuke ili Mkoa wa Singida upate timu kubwa na ndio ilipozaliwa Singida Black Star.

“Lilikuwa jambo kubwa kwa sababu yeye ni mtu wa Mwanza, lakini uwekezaji mkubwa ameufanya Singida,” amesema.

Amesema alkuwa Mwenyekiti wa Wazazi wa Mkoa wa Singida mwaka 2017 hadi 2022 na kipindi ambacho jumuiya hiyo ilifanya makubwa.

“Akiwa jumuiya ya wazazi, ikaanza kuonekana kama jumuiya ya vijana. 2020 aligombea uenyekiti wa Mkoa hakufanikiwa, lakini jina lake ni miongoni mwa yaliyopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa,” amesema.

Ameeleza kiongozi huyo pia aliwahi kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida lakini kura hazikutosha. Ingawa alishindwa, hakulalamika na alionyesha mapenzi kwa chama hicho.

Mwaka jana, amesema walipoanza maboresho ya ofisi ya CCM, alitoa nyumba yake itumike kama ofisi ya muda kwa viongozi wa chama hicho hadi walipomaliza ukarabati.

“Ni mtu aliyeipenda CCM, michezo na jamii. Tumepoteza mtu muhimu sana,” amesema Lissu ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu ya Uongozi katika Elimu, katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Mmoja wa wazee mkoani Singida, Kundya Rajab, ameeleza kushtushwa na taarifa ya kifo cha Mwandami kwa kuwa hakukitarajia, kwani hakuugua bali kimetokea ghafla.

Amesema alimfahamu Mwandami kitambo, tangu alipokuwa mfanyabiashara mdogo hadi anakuwa mkubwa na anamkumbuka kuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuasisi chama cha wachimba madini Singida.

“Namfahamu kuwa mtu aliyejiingiza katika muziki wa Taarab miaka ya nyuma alikuwa na Bendi. Baadaye aliingia kwenye Mpira wa Miguu akiiinua Singida United na aliiwezesha kupata sare na aliinunulia basi,” amesema.

Pia, amesema anamfahamu katika eneo la siasa kwani alikuwa kiongozi katika jumuiya ya wazazi na miaka ya karibuni aligombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida.

Mmoja wa watu wa karibu na marehemu, Idd Abdallah amemwelezea Mwandami kama mtu aliyependa kujichanganya na hakuwa na makuu na watu wengine.

Abdallah amesema mbali na urafiki wa kawaida lakini walikuwa viongozi wote ndani ya CCM Mkoa wa Singida na mipango mingi ilikuwa ikianzia kwa Mwandami.

“Alikuja Singida kama mchimbaji mdogo wa madini, yeye na wenzake wakaanzisha Chama cha Watafiti Madini (wachimbaji wadogo) na kuisaidia Singida na vijana wake kukua kupitia sekta ya madini, akaipenda Singida na akaanza kuwekeza kwa nguvu zote,” amesema Abdallah.

Amesema baadaye, kupitia sekta ya burudani akaanzisha kikundi cha taarab, kikakua na kuwa mfano kwa mkoa huo lakini alithubutu na kuinunua timu ya mpira ya Singida United baada ya kuonekana ikisuasua kutokana na kutelekezwa na mmiliki (mfadhili) wa awali.

“Ikumbukwe aliinunulia timu ya Singida United basi la kisasa na kuwa moja ya vilabu vyenye usafiri wa uhakika na watu walimpenda na kumwamini, hata sisi marafiki zake tulionekana kuwa na heshima kupitia yeye,” amesema.

Kupitia siasa, amesema Mwandami amejijengea hazina kubwa hasa alipokuwa mwenyekiti wa Wazazi mkoa huku akitajwa kama mtu aliyefanya mengi makubwa kupitia pesa na ushawishi wake binafsi.

“Tunapomwomboleza mtu huyu, tukubali aliipenda sana Singida, akawekeza na baadhi ya miundombinu yake imekuwa kioo cha mji na kuinufaisha jamii ya Singida na chama, pia, huyu ndie Yusuf Mwandami,” amesema.

Abdallah ambaye kabla ya kuingia kwenye siasa amekuwa mwandishi na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), ameiomba CCM na Serikali mkoani Singida kumpa heshima stahiki kwani Mwandami hakuwa mtu wa maneno mengi, akisema kwake ilikuwa ni kazi yenye kujali matokeo.

Mchimbaji mdogo wa madini, Maganga Maduhu amemtaja Mwandami kama kiongozi mwenye kuonyesha njia na hasa katika mafanikio kwa mtu anayejishughulisha kwa kazi halali.

Maduhu amesema alifahamiana na Mwandami kwa zaidi ya miaka 19 alipokuwa akifanya kazi kwenye moja ya mashimo yake ya madini.

“Aliyekupa namba yangu hajakosea, huyu bwana tunafahamiana kwa muda mrefu sana, naweza kusema hata huku niliko (Katavi) ni juhudi zake, huyu jamaa lazima nikashuhudie maziko yake,” amesema Maduhu.

Kwa mujibu wa mchimbaji huyo, hakuwahi kusikia kama ndugu huyo alikuwa na shida wala changamoto ya aina yoyote kwenye afya hadi aliposikia taarifa za kifo.

Asha Chuli ambaye aliwahi kufanya kazi katika moja ya vitega uchumi vya marehemu, amesema katika kipindi cha miaka miwili na miezi saba aliyofanya kazi hapo, hakuwahi kukwazana naye na wakati wote alipenda utani.

Hata hivyo, amesema enzi za uhai wake, Mwandami alikuwa mkali kwenye biashara akisisitiza kauli nzuri kwa wateja na kwamba angekuwa tayari kumsamehe mtu aliyemuibia kuliko mtu anayetoa lugha chafu kwa wateja.