TPDC: Kuna mafuta yakutosha miezi mitatu, yatapanda bei

Dar es Salaam. Serikali imesema Tanzania ina hifadhi ya mafuta yanayoweza kutumiwa kwa miezi mitatu kuanzia Mei hadi Julai mwaka huu, huku ikiweka bayana kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ndiyo litakalo sambaza mafuta kwa kipindi hicho.

Hiyo ni baada ya TPDC kupata wasambazaji wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa gharama nafuu kuliko wale waliopatikana kupitia Wakala wa Ununuzi wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

Hayo yamewekwa wazi huku Watanzania wakitakiwa kujiandaa kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta Tanzania, baada ya bei ya jumla kuongezeka.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayesimamia sekta ya Nafuta, Dk Jamea Mataragio, amesema hayo leo, Machi 28, 2026, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.

Akitoa takwimu za mafuta yaliyopo, Dk Mataragio amesema jumla ya mafuta ya petroli yatakayokuwapo nchini kwa kipindi hicho ni lita 380.6 milioni, ambayo yanatosha kwa siku 61.

Pia, amesema kupitia mikataba ya uagizaji wa mafuta ambayo Tanzania imeingia, lita 183.5 milioni za mafuta zinatarajiwa kufika Aprili mwaka huu.

“Hii itaifanya Tanzania kuwa na jumla ya lita 563.68 milioni za petroli, ambazo yatatosha kwa siku 91,” amesema Dk Mataragio.

Kwa upande wa dizeli, amesema akiba iliyopo ni lita 55.74 milioni, yaliyowasili ni lita 122.8 milioni, na yaliyo njiani ni lita 184.62 milioni.

Amesema hii inafanya jumla ndogo kuwa lita 362.46 milioni, ambazo zinatosha kwa siku 44.

“Pia, mafuta ya mikataba yaliyopo njiani ni lita 167.32 milioni, ambayo inafanya jumla ya lita 530.621 milioni,” amesema.

Mafuta ya ndege yaliyopo ni lita 35.24 milioni, na yaliyo katika mikataba ni lita 23.7 milioni, ambayo yanafanya jumla ya lita 59.2 milioni, zinatosha kwa siku 97.

 “Tuna mafuta ya kutosha miezi mitatu, na bei itakuwa himilivu, japokuwa tunatarajia zitapanda kwa sababu bei duniani inaongezeka,” amesema.

Akizungumzia ongezeko la bei katika soko la dunia, amesema wakati vita ya Marekani, Israel, na Iran inaanza Februari mwaka huu, pipa moja lilikuwa kati ya Dola 50–60 za Marekani, na sasa ni Dola 114 za Marekani kwa pipa, ambayo ni mara mbili ya bei ya awali.

“Hivyo, tutegemee mafuta yapande, ila bei itakuwa himilivu,” amesema.

Amesema hayo ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu kuanza kwa vita katika ukanda wa Mashariki ya Kati, vinavyohusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambavyo vinatishia hatari ya kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo katika nafasi ya kukumbwa na hatari hiyo, kwani baadhi ya nchi zilizoathiriwa ndizo chanzo kikuu cha mafuta yanayoagizwa nchini.

Mvutano huu tayari umeanza kuathiri mwenendo wa soko la kimataifa, hali inayoongeza wasiwasi wa kupanda kwa gharama za usafirishaji, uzalishaji, na maisha ya kila siku kwa wananchi.

Akielezea kwa nini TPDC itasambaza mafuta hayo, amesema uchambuzi uliofanyika kwenye masoko ya mafuta na kuangalia gharama ndiyo uliamimua.

Amesema PBPA aliwasiliana na wadau na waagizaji wa mafuta walikuja na bei zilizokuwa juu zaidi ya mara mbili ya gharama.

Amesema TPDC alipoingia sokoni na kuzungumza na wazalishaji na wasambazaji, alipata gharama nafuu ya Dola 100 za Marekani, ukilinganisha na gharama walizopata PBPA, ambayo ingefanya gharama kuwa juu zaidi.

“Tumebaini kuwa upatikanaji wa mafuta ni mgumu, hasa unapoagiza mzigo mdogo, bei inakuwa kubwa. Ili upate bei nzuri na uweze kupata mkataba mzuri, unatakiwa kuwa na kiwango kikubwa cha uhitaji wa mzigo,” amesema.

Pia, ni lazima uwe na mkataba wa muda mrefu na uweze kusaini mkataba kuhakikisha unachukua mafuta kwa muda huo.

“TPDC walichukua mzigo kwa sababu wana mamlaka kisheria ya kufanya hivyo, ili kuhakikisha nchi ina usalama wa mafuta,” amesema.

Jambo hilo litaifanya TPDC kuwa na mamlaka ya kusimamia usambazaji wa mafuta kuanzia Mei hadi Julai, kwa sababu walipata bei nzuri.

“Ni hatua ambayo Serikali imechukua kuhakikisha kunakuwepo na mafuta hadi Julai,” amesema.

“Na tutahakikisha mafuta yanafika vituoni, kwani kuna taarifa kuwa baadhi ya watu wanaingia katikati ili kumshawishi ‘supplier’ kuuza nchi nyingine.

Katika hatua za muda mrefu, amesema wamejipanga kuhakikisha nishati ya gesi iliyopo nchini inatumika kikamilifu.

Amesema Tanzania inaendelea kuhakikisha utafutaji wa mafuta na gesi unafanyika katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Eyasi, Wambele, na kuendeleza kitalu cha Mnazi Bay, Songosongo, na visima vitatu vinavyochorongwa sasa.

Hilo linalenga kuhakikisha nchi inaongeza gesi wakati miundombinu ya kusambaza gesi ikiendelea.

“Tuna bomba la kilometa 35 kutoka Ntorya kwenda Madimba, na hadi mwakani tutakuwa tumeongeza futi za ujazo 100 milioni ambazo zitaongezwa upande wa mkondo wa kati,” amesema.

“Lilo limeenda sambamba na ujenzi wa vituo vya kujazia gesi katika maeneo mbalimbali vilivyofika 11, huku magari ya kuuza gesi (mobile CNG) yakiwa mbioni kununuliwa kwa ajili ya Dodoma na Arusha,” amesema.

Kuhusu mipaka, amesema wameshirikiana na vyombo vya ulinzi kudhibiti ulanguzi unaofanyika, ili kuhakikisha mafuta yaliyopo nchini yanatumika ndani ya nchi pekee.

Ametumia nafasi hiyo kuonya watu wachache wasiokuwa waaminifu, wanaochukua mafuta mengi kuliko mahitaji na kuficha kusubiri bei ipande ili wauze.

“Kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi. Ukikamatwa, utashtakiwa. Niwaombe wote wanaofanya hivyo waache mara moja; wanatengeneza uhaba bandia,” amesema.

Ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutomuonea mtu aibu, ili kuhakikisha mafuta yanayopakiwa Dar es Salaam yanafika katika vituo vilivyopagwa.

Kamishna wa Mafuta na Gesi wa Wizara ya Nishati, Goodluck Shirima, amesema Serikali itaendelea kusimamia sekta, licha ya kuwa duniani mafuta yamepanda, jambo linaloendana na Tanzania.

“Tuko macho kwenye vituo na depo, kuhakikisha mafuta yote yanafika vituoni, ili wananchi wapate mafuta bila changamoto yoyote,” amesema.