Wahouthi waishambulia Israel, vita Mashariki ya Kati vyazidi kupanuka

Waasi wa Kihouthi wa Yemen wanaoiungwa mkono na Iran wamerusha makombora kuelekea Israel leo Jumamosi, likiwa ni shambulizi lao la kwanza tangu kuanza kwa vita kati ya Iran na Marekani pamoja na Israel.

Wakati hayo yakitokea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema nchi yake inatarajia kukamilisha operesheni za kijeshi ndani ya wiki chache.

Kundi la Wahouthi, ambalo kuhusika kwake kunaweza kupanua na kurefusha vita vilivyoingia wiki ya tano, limesema mashambulizi yao yataendelea hadi kile walichokiita “uchokozi” kwenye pande zote kitakapokoma.

Hata hivyo, Israel imesema imefanikiwa kuzuia kombora hilo lililorushwa kutoka Yemen.

Vita hivyo vilivyoanza Februari 28, 2026 kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran na yenyewe ikijibu mashambulizi, vimesambaa kote Mashariki ya Kati, vikisababisha vifo vya maelfu ya watu na kuathiri usambazaji wa nishati duniani, jambo linaloelekea kuyumbisha uchumi wa dunia na kuongeza hofu ya mfumuko wa bei.

Wahouthi walisema jana, Ijumaa kuwa wako tayari kuchukua hatua iwapo ongezeko la mashambulizi dhidi ya Iran na “Muungano wa Upinzani” utaendelea katika vita hivyo.

Kundi hilo limeonyesha uwezo wa kushambulia malengo yaliyo mbali na Yemen pamoja na kuvuruga njia za usafirishaji wa baharini katika Rasi ya Arabia na Bahari Nyekundu, kama walivyofanya kuunga mkono Hamas huko Gaza baada ya Oktoba 7, 2023.

Iwapo Wahouthi watafungua uwanja mpya wa mapambano, shabaha kuu inaweza kuwa Mlango Bahari wa Bab al-Mandab, njia muhimu ya usafirishaji inayodhibiti meli zinazoelekea Mfereji wa Suez, hasa baada ya Iran kufunga kwa kiasi kikubwa Mlango Bahari wa Hormuz.

Akizungumza kabla ya shambulizi hilo, Rubio amesema Marekani iko “ndani au mbele ya ratiba” na inatarajia kumaliza operesheni za kijeshi “ndani ya wiki, si miezi.”

Pia, amewaambia mawaziri wa nchi za kundi la G7 nchini Ufaransa kwamba nchi za Ulaya na Asia zinazofaidika na biashara kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, zinapaswa kuchangia juhudi za kuhakikisha njia hiyo inabaki wazi, kwani hupitisha takriban theluthi moja ya mafuta na gesi asilia ya dunia.

Vita hivyo, pia, vimezua mgawanyiko kati ya Marekani na washirika wake wa jadi ambao wamechagua kubaki pembeni.

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema ukosefu huo wa msaada unaweza kuwa na athari kwa Nato, muungano muhimu wa kijeshi wa Magharibi.

Masoko ya hisa yaliporomoka kwa kasi Ijumaa iliyopita kutokana na hofu kuwa vita vitaendelea kwa muda mrefu, huku bei ya mafuta ghafi ya Brent ikivuka dola 112 kwa pipa—ongezeko la zaidi ya asilimia 50 tangu vita vilipoanza.

Nchini Marekani, ambako Trump anakabiliwa na shinikizo la kisiasa kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, bei ya dizeli katika jimbo la California ilifikia wastani wa juu zaidi kuwahi kurekodiwa wa dola 7.17 kwa galoni, kulingana na Chama cha Magari cha Marekani (AAA).

Trump ameonekana kutaka kumaliza haraka vita hivyo visivyopendwa na wananchi, akisisitiza kile alichokiita mazungumzo yenye tija na Iran, yanayolenga kupata suluhisho la kidiplomasia.

Nchi za Pakistan, Misri na Uturuki zimekuwa zikipitisha ujumbe kati ya pande zinazopigana, ingawa Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa hakuna mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.

Vyanzo viwili vinavyofahamu juhudi hizo za nyuma ya pazia, vina mashaka kuwa mazungumzo ya moja kwa moja yatafanyika hivi karibuni.

Alhamisi, Trump aliongeza muda wa siku 10 kwa Iran kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz, la sivyo ikabiliwe na mashambulizi dhidi ya vituo vya umeme na miundombinu ya nishati. Ingawa mashambulizi hayo yalisitishwa kwa muda, huku Marekani na Israel zimeendelea kuishambulia Iran.

Iran ilirusha mawimbi kadhaa ya makombora kuelekea Israel usiku, yakimuua mtu mmoja na kusababisha milipuko kadhaa katika eneo la Tel Aviv kutokana na mabomu ya kusambaa na mabaki ya makombora yaliyozuiwa.

Shambulizi la Iran dhidi ya kambi ya kijeshi nchini Saudi Arabia liliwajeruhi wanajeshi 12 wa Marekani, wawili wakiwa mahututi, ofisa mmoja wa Marekani aliiambia Reuters huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yakiendelea katika ukanda wa Ghuba.

Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain zimeripoti mashambulizi ya makombora mapema Jumamosi, ambapo watu watano walijeruhiwa na moto kuzuka baada ya kombora kuzuiwa karibu na Bandari ya Khalifa mjini Abu Dhabi, mojawapo ya bandari kubwa za makontena katika eneo hilo.

Watu wasiopungua watano waliuawa na wengine saba kujeruhiwa kufuatia shambulizi la Marekani na Israel kwenye makazi ya watu katika mji wa Zanjan kaskazini-magharibi mwa Iran, vyombo vya habari vya Iran viliripoti. Pia, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran kilichopo Tehran kiliripotiwa kushambuliwa.