CRDB Bank kupitia Kitengo chake cha Manunuzi (Procurement) imetembelea Makao ya Taifa ya Kulelea Watoto yaliyopo Kikombo, Ihumwa jijini Dodoma, na kutoa msaada wa mahitaji muhimu kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha ustawi wa jamii.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika kituo hicho, Mkuu wa Manunuzi – Mikataba, Udhibiti na Uzingatiaji wa CRDB Bank, Victor Mukami, amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea hali halisi ya maisha ya watoto hao, kujifunza pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa benki hiyo wa kuhakikisha inabaki kuwa karibu na jamii, wadau wake pamoja na makundi yenye uhitaji, kupitia utekelezaji wa sera ya kurejesha kwa jamii (Corporate Social Responsibility – CSR).
“Tumekuja hapa Kikombo kuona kwa karibu hali halisi ya kituo hiki katika ngazi ya kitaifa, kujifunza na kubadilishana mawazo. Hii si mara ya mwisho, tutaendelea kutembelea vituo mbalimbali nchini,” amesema Mukami.
Aidha, Mukami ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia vituo vya kulelea watoto, akisisitiza kuwa bado kuna mahitaji makubwa yanayohitaji ushirikiano wa pamoja kutoka kwa jamii.
Pia amewasihi wazazi na walezi kuendelea kuwaonesha watoto upendo na malezi bora, akibainisha kuwa upendo una mchango mkubwa katika ukuaji wao wa kiakili na kisaikolojia.
Kwa upande wake, Meneja wa Makao hayo, Darius Karijongo, ameishukuru CRDB Bank kwa msaada huo, akisema kuwa ujio wao umeleta faraja kubwa kwa watoto pamoja na uongozi wa kituo hicho.
“Tunawashukuru sana CRDB Bank kwa kujitokeza kutuunga mkono. Hawa watoto wanahitaji upendo ambao hawakupata kutoka kwa familia zao za karibu. Sisi sote ni familia yao sasa,” amesema Karijongo.
Ameongeza kuwa msaada uliotolewa una thamani kubwa kwa maendeleo ya kituo hicho, na kuahidi kuwa utatumika ipasavyo kwa manufaa ya watoto hao.
“Leo mmetuonesha kuwa ninyi ni ndugu zetu wa karibu. Tunawashukuru sana kwa zawadi mlizotupatia, Mungu awabariki,” ameongeza.
Ziara hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya CRDB Bank katika kuendelea kugusa maisha ya Watanzania na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.