Chakuhawata chalia kubaguliwa kikihusishwa na vyama vya upinzani

Dodoma. Chama cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania (Chakuhawata) kimesema kimekuwa kikinyimwa fursa za kushiriki katika masuala mbalimbali ya kitaifa yanayohusu wafanyakazi, ikiwemo maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) na mabaraza ya wafanyakazi, kwa madai ya kufananishwa na vyama vya siasa vya upinzani.

Akizungumza leo, Jumamosi, Machi 28, 2026 jijini Dodoma katika kikao cha Kamati Tendaji Taifa, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Abisias Lutandika, amesema mtazamo huo si wa kweli, kwani chama hicho ni halali na kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria.

“Kwa mfano, hatupewi taarifa za maadhimisho ya Mei mosi, na hata tunapojaribu kushiriki, tunaondolewa kwenye maandamano. Pia, hatushirikishwi kwenye mabaraza ya wafanyakazi yanayojadili masuala muhimu ya wafanyakazi,” amesema Lutandika.

Ameeleza kuwa sababu kubwa ya hali hiyo ni dhana potofu inayowafanya waonekane kama chama cha kisiasa, jambo alilosisitiza si sahihi.

Chama hicho kilianzishwa mwaka 2015 mkoani Kigoma kikiwa na wajumbe 182, na hadi Februari 2026 kilikuwa na wanachama 49,750 nchi nzima.

Lutandika ametaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri kutotoa ushirikiano, hasa katika suala la makato ya michango ya wanachama.

Amesema baadhi yao hushindwa kuwasilisha makato hayo au kuwakatia wafanyakazi mara mbili, hali inayosababisha malalamiko miongoni mwa wanachama.

Kutokana na hali hiyo, amependekeza Serikali kuweka utaratibu kwenye mfumo wa ESS Utumishi utakaowawezesha wafanyakazi kujiunga na vyama wanavyovitaka moja kwa moja bila kupitia waajiri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Anuai za Jamii kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mwanaamani Mtoo, amekitaka chama hicho kuendelea na shughuli zake bila hofu, huku akiahidi kuwa Serikali inafanyia kazi changamoto zote zilizobainishwa.

“Uwepo wa chama hiki tangu mwaka 2015 hadi sasa unaonesha kinakubalika. Serikali inaendelea kushughulikia changamoto mlizozieleza, hivyo endeleeni kutekeleza majukumu yenu bila wasiwasi,” amesema Mtoo.

Aidha, amesisitiza kuwa kikao hicho kiwe fursa kwa wanachama kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha chama hicho ili kiweze kutimiza malengo yake ya kutetea haki na maslahi ya walimu nchini.

Naye mwakilishi wa wanawake wa chama hicho, Novemba Mguwili, amesema zaidi ya wajumbe 120,000 kutoka wilaya 84 zilizokamilisha uchaguzi wamehudhuria kikao hicho, huku wilaya 44 zikiwa bado hazijafanya uchaguzi.

Amesema kikao hicho ni jukwaa muhimu kwa wanachama kujadili namna bora ya kulinda na kutetea haki za walimu pamoja na kuishauri Serikali katika kuboresha maslahi yao.