Pedro atuma ujumbe Yanga | Mwanaspoti

WAKATI Yanga ikijipanga kurejea mazoezini kesho Jumatatu, kocha wa kikosi hicho Pedro Goncalves, ameweka wazi hesabu zake juu ya mastaa watano wa timu hiyo, huku akikiri kwamba kurejea kwao utaimarisha zaidi kikosi.

Yanga imeingia na mguu mbaya msimu huu kwa janga la wachezaji majeruhi ambalo limeendelea kuitafuna timu hiyo ikiwa na wachezaji nane majeruhi ambapo watatu ni kama wamemaliza msimu tayari ambao ni Khomein Abubakar, Dickson Job na Clement Mzzie, huku Laurindo Depu, Prince Dube, Edmund John, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Chadrack Boka majeraha yao yakiwa ya muda mfupi na wanaweza kucheza mechi zinazofuatia. Mbaya zaidi, orodha hiyo ya majeruhi, asilimia kubwa ni wale wanaocheza kikosi cha kwanza ukimuondoa Edmund na Khomein.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema kama wachezaji walioko majeruhi watarudi hata watano tu wakiwa imara, basi timu hiyo itakuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye maeneo yote.

“Yanga itarudi kwenye ubora wake kutokana na kurejea kwa wale waliokuwa majeruhi ambao wanakuja kuimarisha kila idara kuanzia ulinzi, kiungo na safu ya ushambuliaji.

“Wakirejea Ibrahim Bacca, Depu, Dube, Edmund na Boka, basi timu itakuwa bora, ni wazi hawa ni wachezaji muhimu katika kila sehemu uwanjani na mchango wao ni mkubwa, hivyo kuwakosa ni mtihani mgumu sana.

“Majeruhi ni tatizo kubwa lililotuondolea ubora uwanjani, nimefurahia mapumziko ya kalenda ya kimataifa yamesaidia sana wachezaji wetu kupumzika kabla ya Jumatatu kuanza mazoezi rasmi tukijiandaa na mchezo wa ligi,” alisema Pedro. Kocha huyo raia wa Ureno, aliongeza kuwa: “Yanga bado ipo salama na ina nafasi kubwa ya kushinda ubingwa kuliko kuukosa licha ya matokeo ambayo tumeyapata mechi za karibuni, imani yetu na malengo ya ubingwa yako palepale.”

Baada ya ligi kusimama kupisha kalenda ya FIFA, Aprili 4 mwaka huu Yanga itaikaribisha Tanzania Prisons katika mwendelezo wa ligi hiyo ambayo Wanajangwani hao wanaongoza msimamo kwa pointi 38 wakicheza mechi 16, wakishinda 11 na sare tano.