MAHUBIRI: Kanuni tano za Kimungu kushinda tamaa za mwili

Wapendwa katika Kristo, Bwana Yesu asifiwe. Leo tunaangalia somo muhimu katika maisha ya Mkristo: jinsi ya kushinda tamaa ya mwili. Ukweli ni kwamba tamaa ya mwili ina nguvu, hasa kwa mtu ambaye hajaokoka kikamilifu au hajamruhusu Mungu kutawala maisha yake yote.

Tamaa hizi zinaweza kumfanya mtu aishi maisha ya kushindwa, hatia na kujitenga na Mungu, lakini habari njema ni kwamba ushindi unawezekana!

Yapo mambo kadhaa yanayoweza kuchochea mtu kujikuta katika tamaa za mwili: hali ya uchumi. Kuna mtu anakuwa na hali ngumu ya maisha, anaona njia rahisi ya kupata kipato ni kujiingiza kwenye uasherati na uzinzi.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia. Siku hizi ni rahisi watu kuwasiliana kupitia njia za kisasa, hasa mitandao ya kijamii, na kurahisisha watu kuongea, kutumiana picha na video chafu.

Saikolojia ya mtu, jamii au kabila. Hii hutokana na kurithi vinasaba katika ukoo au familia na kujikuta katika mwendelezo wa waliotangulia.

Hivyo basi, tunawezaje kushinda tamaa ya mwili? Hebu tuangalie kanuni hizi tano muhimu.

Kukiri kuwa Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi kwa kumaanisha

Hatua ya kwanza na ya msingi kabisa ni kumpokea Yesu Kristo kwa dhati moyoni mwako. Sio kusema kwa mdomo tu, bali kumaanisha kutoka ndani ya moyo wako. Unapofanya hivyo, Roho wa Mungu anaingia ndani yako na kuanza kazi ya kubadilisha maisha yako.

Biblia inasema katika 1 Yohana 4:15: Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu.

Hii ina maana kuwa huwezi kushinda tamaa ya mwili kwa nguvu zako mwenyewe. Unahitaji uwepo wa Mungu ndani yako. Roho Mtakatifu ndiye anayekupa nguvu ya kusema hapana kwa dhambi na ndiyo kwa haki.

Yesu alifundisha wazi kuwa mtu yeyote anayetaka kumfuata lazima ajikane mwenyewe. Kujikana ni kukataa tamaa zako mbaya, hata kama zinaonekana tamu au za kuvutia machoni.

Hapa ndipo mapambano ya kweli yalipo. Mwili unataka kufanya dhambi, lakini roho inataka kumpendeza Mungu. Hivyo, lazima uchague. Kujikana ni kusema: “Sitafuata hisia zangu, nitafuata mapenzi ya Mungu.”

Hii ni vita ya kila siku. Ni uamuzi wa kila wakati. Hivyo, kadri unavyoendelea kujikana, ndivyo unavyozidi kuwa na nguvu ya kiroho.

Kujaza neno la Mungu ndani yako

Neno la Mungu ni silaha yenye nguvu sana dhidi ya tamaa ya mwili. Usipokuwa na Neno ndani yako, utakuwa dhaifu kiroho. Lakini ukijaa Neno, unakuwa na nguvu ya kushinda majaribu.

Zaburi 119:11 inasema: Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi.

Hii inaonesha dhahiri kuwa neno la Mungu lina uwezo wa kumzuia mtu asianguke dhambini. Unapojifunza Biblia, kuisoma kila siku na kuitafakari, akili yako inabadilika. Mawazo yako yanakuwa safi, na tamaa za mwili zinaanza kupungua.

Kuwa mtu wa maombi mara kwa mara

Maombi ni nguvu kubwa sana katika maisha ya Mkristo. Ni mawasiliano yako na Mungu. Ni mahali ambapo unapata nguvu mpya na ushindi juu ya tamaa za mwili.

Maombi ni kama upanga wa Roho. Yanaua tamaa za mwili na kukupa ushindi. Usingoje mpaka unapokuwa kwenye shida ndipo uombe. Fanya maombi kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku.

Omba kwa roho na kwa kweli. Omba hata wakati hujisikii. Kadri unavyoomba, ndivyo unavyozidi kuwa na nguvu ya kiroho.

Maombi ya nguvu na mamlaka

Kuna nyakati ambapo tamaa fulani za mwili zinakuwa sugu sana. Unaweza kupambana nazo kwa muda mrefu bila ushindi.

Baadhi ya matatizo ya mwili si ya kawaida, yanaweza kuwa ni mapando ya adui au hata kurithi. Hivyo, yanahitaji maombi ya nguvu ili kung’olewa.

Yesu alisema katika Mathayo 15:13: Kila pando alilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang’olewa.

Hii ina maana kuwa chochote kisicho cha Mungu ndani ya maisha yako kinaweza kuondolewa kwa nguvu za Mungu.

Ukifuata kanuni hizi kwa uaminifu, utaona mabadiliko makubwa katika maisha yako. Tamaa za mwili hazitakuwa tena na nguvu juu yako. Utaishi maisha ya ushindi, utakatifu na kumpendeza Mungu.

anapatikana 0789418612 kwa maombi na ushauri.