……………
Na Carlos Claudio, Dodoma.
CHAMA cha kutetea na kulinda haki za walimu nchini (CHAKUWAHATA) kimeiomba Serikali kuingilia kati na kutoa maelekezo mahsusi kwa waajiri wa walimu, hususan Wakurugenzi wa Halmashauri, ili kuhakikisha walimu wanapatiwa uhuru wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi bila vikwazo.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 28, 2026 jijini Dodoma na Mbunge na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Abisias Lutandika, wakati wa kikao cha Kamati Tendaji ya Taifa kilichokutana kujadili masuala mbalimbali yanayokihusu chama hicho.
Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa chama hicho, bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazodhoofisha juhudi za kulinda na kutetea maslahi ya walimu.
“Tunaiomba Serikali itoe maelekezo kwa waajiri kuwapa uhuru wafanyakazi kujiunga na vyama wanavyovipenda. Hii ni haki ya msingi ya mfanyakazi ambayo inapaswa kulindwa,” amesema Lutandika.
Amefafanua kuwa baadhi ya waajiri wamekuwa wakikwamisha zoezi la uandikishaji wanachama kwa kuchelewesha au kutotekeleza makato ya ada za uanachama licha ya walimu kukamilisha taratibu zote za kisheria.
Aidha, baadhi ya halmashauri zimekuwa haziishirikishi CHAKUWAHATA katika mabaraza ya wafanyakazi, jambo linalowanyima wanachama wake uwakilishi muhimu katika maamuzi ya kikazi.
Changamoto nyingine zilizotajwa ni pamoja na kuwahamisha walimu viongozi wa chama bila sababu za msingi, kucheleweshwa kwa stahiki zao za uhamisho, pamoja na kuwepo kwa makato ya vyama viwili kwenye mishahara ya baadhi ya wanachama kinyume cha sheria.
Pia, chama hicho kimeeleza kusikitishwa na baadhi ya wanachama wake kutoshirikishwa katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), huku wengine wakidai hata kuondolewa kwenye maandamano wanapojitokeza kushiriki.
Kwa mujibu wa Lutandika, vitendo hivyo vinadhoofisha ari ya walimu kujiunga na chama hicho na vinakiuka misingi ya haki na usawa kazini.
Katika mapendekezo yao, CHAKUWAHATA imeiomba Serikali kuingiza vyama vya wafanyakazi katika mfumo wa kielektroniki wa utumishi (ESS) ili kurahisisha mchakato wa kujiunga au kujiondoa kwenye vyama bila kuingiliwa na waajiri.
“Utaratibu huu utapunguza usumbufu na malalamiko kutoka kwa wafanyakazi, na kuweka uwazi katika mchakato mzima,” alisisitiza.
Awali akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais, Mwanaamani Juma Mtoo, amesema Serikali inatambua umuhimu wa vyama vya wafanyakazi na imejipanga kushughulikia changamoto zinazowakabili ili kuboresha mazingira ya kazi.
Amesema hatua mbalimbali tayari zinaendelea kuchukuliwa kushughulikia changamoto hizo na kusisitiza kuwa uwepo wa changamoto ni sehemu ya mchakato wa maendeleo.
“Tunatambua mchango wa vyama vya wafanyakazi katika kulinda haki za watumishi. Serikali itaendelea kushirikiana nanyi ili kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi,” amesema Mtoo.
Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa Kamati Tendaji wameeleza matumaini yao kuwa Serikali itachukua hatua za haraka ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uhuru wa walimu katika kuchagua vyama vyao.
Taarifa zinaonyesha kuwa tangu kuanzishwa kwa CHAKUWAHATA, chama hicho kilianza na wanachama 182 kutoka Manispaa ya Kigoma/Ujiji na sasa kimepanua wigo wake hadi kufikia halmashauri mbalimbali nchini.
Tayari kimefanya uchaguzi wa viongozi katika wilaya 84 na kinatarajia kufanya uchaguzi katika wilaya 44 zaidi zilizokidhi vigezo vya kikatiba.
Hatua hiyo inaonesha kukua kwa chama hicho, licha ya changamoto zinazokikabili katika safari ya kutetea haki za walimu nchini.







