MKURUGENZI WA TET DK KOMBA AFUNGA KIKAO CHA MAANDALIZI YA ‘KALIMANI APP’

 ******

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt Aneth Komba leo tarehe  27/3/2026 amefunga rasmi kikao kazi cha siku tatu cha kuandaa maudhui ya Kuhesabu katika “Kalimani App” kwa kutumia  Mtaala ulioboreshwa  wa Mwka 2023 na Kamusi ya Lugha ya Alama ya Tanzania.

 App hiyo inaandaliwa kwa ajili wanafunzi viziwi wa Darasa la Awali, la Kwanza na la Pili. Kikao Kazi hicho kilichofanyika  katika Hotel ya Protea iliyopo jijini ,Dar es Salaam.

Akifunga kikao kazi hicho Mkurugenzi Mkuu Dkt. Komba amesema, maboresho ya Sera ya  Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 yemejikita katika kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa ni jumuishi na kuwa hakuna mtoto hata mmoja anayeachwe.

 “Wazazi wenye watoto wenye mahitaji maaalum naomba muwapeleka  shuleni kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeandaa mazingira wezeshi kwa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu.”amesema Dkt.Komba

Pia , amewashukuru Jenga Hub kwa maono na ubunifu wao katika kuandaa App hiyo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kisayansi wa KKK, uliozinduliwa na Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni. 

Vilevile, ameeleza kuwa TET itashirikiana kwa ukaribu na Jenga Hub kuhakikisha kuwa lengo la kuandaa App linafikiwa na kuwa App hiyo inawanufaisha walengwa wote nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jenga Hub iliyobuni Kalimani App, Bi Nancy Sumari, ameeleza kuwa  App hiyo  imelenga kutumiwa na  watoto viziwi wa Darasa la Awali, Darasa la Kwanza, Pili na la Tatu.

Aidha, ameeleza kuwa Kalimani App inaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Jenga Hub na TET kuwa  itawawezesha watoto viziwi kujifunza Kuhesabu kwa urahisi na hivyo kuhakikisha lengo la serikali la  kuwawezesha wanafunzi kuweza kuhesabu  kwa ufasaha kabla ya kufika Darasa la Tatu linafikiwa. 

Hata hivyo ,Bi Nancy ameishukuru  TET kwa kuwa tayari kushirikiana  na taasisi ya Jenga Hub  katika kuhakikisha kuwa watoto viziwi  nao wanapata haki yao ya msingi ya kupata vifaa vya kufundishia na kujifunzia.