Canada. Utamaduni wa harusi una sura nyingi – nyingine za kushangaza, nyingine za kutia tabasamu.
Katika kona mbalimbali za dunia, ndoa si tukio la kuvaa pete na kula keki pekee. Ni tamasha la mila, imani na desturi zinazorithishwa kizazi hadi kizazi. Baadhi ya mila hizo ni za kipekee kiasi cha kuwafanya wengi kubaki midomo wazi. Leo, tunaangazia baadhi ya sherehe za ndoa za ajabu na za kuvutia kutoka jamii tofauti duniani.
Kupakwa rangi na masizi – Scotland
Katika baadhi ya maeneo ya Scotland, marafiki wa bwana harusi (na wakati mwingine bibi harusi) huwapaka mchanganyiko wa rangi nyeusi, masizi, manyoya, maziwa yaliyoganda na unga. Tukio hili la hadharani huaminika kuwaandaa wanandoa kwa changamoto za maisha ya ndoa kwa kuwajengea uvumilivu.
Bibi harusi kulia kwa mwezi mzima – China
Kwa jamii ya Tujia nchini China, bibi harusi hulazimika kulia kwa saa moja kila siku kwa mwezi mzima kabla ya harusi. Baadaye, mama, bibi na dada zake hujiunga naye katika kilio hicho kama ishara ya shukrani na maandalizi ya maisha mapya.
Kununa badala ya kucheka – DRC
Katika baadhi ya maeneo ya Kongo, wanandoa hawaruhusiwi kucheka wakati wa harusi. Kununa ni ishara ya uzito wa jukumu la ndoa na huchukuliwa kama dalili ya umakini.
Kuolewa na mti kuondoa laana – India
Baadhi ya wanawake wanaozaliwa chini ya hali maalumu ya unajimu iitwayo Manglik dosha, huozwa kwanza na mti, mara nyingi mgomba, ambao hukatwa baadaye. Mila hii huaminika kuondoa mkosi kabla ya ndoa halisi.
Kupigwa samaki kuthibitisha ushupavu – Korea Kusini
Baada ya harusi, marafiki humfunga bwana harusi kifundo cha mguu na kumpiga nyayo kwa samaki waliokauka. Kitendo hiki cha kipekee huchukuliwa kama jaribio la kuthibitisha uimara wake wa kimwili na kiakili.
Kuvunja vyombo kuashiria umoja – Ujerumani
Katika mkesha wa harusi, marafiki huvunja vyombo vya udongo, kisha wanandoa husafisha pamoja. Mila hii, ijulikanayo kami Polterabend,
huashiria umoja katika kukabiliana na changamoto. Kioo ni mwiko kuvunjwa kwani huaminika kuleta mkosi.
Kwa jamii ya Wamasai, baba humtemea binti yake mate kichwani na kifuani kabla ya kuondoka kuolewa. Hii ni ishara ya baraka na heri. Bibi harusi haruhusiwi kutazama nyuma ili kuepuka kuvuruga bahati yake.
Kuoshwa kwa maua – Indonesia
Katika jimbo la Java, bibi harusi huoshwa na wazee wa familia kwa maji yenye maua kama ishara ya utakaso na maandalizi ya maisha mapya ya ndoa.
Mabusu ya wazi – Sweden
Nchini Sweden, furaha huonyeshwa waziwazi. Bwana harusi akiondoka kidogo, wageni wa kiume hupanga mstari kumbusu bibi harusi; naye bibi harusi akitoka, wanawake humbusu bwana harusi. Ni utamaduni unaochukuliwa kwa mzaha na furaha.
Kutekwa kwa bibi harusi – Romania
Marafiki wa bibi harusi humteka kwa muda na kumficha hadi bwana harusi ajadiliane au alipe fidia. Mila hii hupima utayari wake wa kumrejesha mke wake.
Asali na mlozi kwa baraka – Ugiriki
Katika harusi za Kigiriki, rafiki wa karibu wa bwana harusi humnyoa ndevu kama ishara ya uaminifu. Baadaye, wanandoa hulishwa asali na mlozi kuashiria maisha matamu na yenye mafanikio.
Katika mila iitwayo Joota Chupai Kaskazini mwa India, ndugu wa bibi harusi huiba kiatu cha bwana harusi na kumtaka atoe dau ili kukirejesha. Ni ushindani wa kirafiki unaoleta burudani.
Uchunguzi wa ini la kuku – Mongolia
Kabla ya ndoa, kuku huchinjwa na ini lake kuchunguzwa. Lisipoonekana kuwa na afya njema, huchinjwa mwingine hadi lipatikane linalofaa ikiwa ni ishara ya kutabiri mustakabali wa ndoa.
Mchele na kichanga kitandani – Czech Republic
Katika mila za zamani za Chekoslovakia (leo Czech Republic na Slovakia), marafiki huweka mtoto mdogo kitandani mwa wanandoa kuashiria baraka ya watoto. Nafaka na mchele hutawanywa kuonyesha neema na ustawi.
Vikombe vitatu vya sake – Japan
Katika sherehe ya San-San-Kudo, wanandoa hunywa sake mara tisa kutoka vikombe vitatu. Kitendo hiki huunganisha rasmi familia mbili na kuchukuliwa kuwa cha baraka zaidi kuliko viapo vya maneno.
Kunenepeshwa kwa maandalizi – Africa Magharibi
Katika baadhi ya jamii za Afrika Magharibi, bibi harusi huwekwa katika vibanda maalumu na kulishwa ili anenepe kabla ya ndoa. Unene huonekana kama ishara ya uzuri, ustawi na uwezo wa kuzaa watoto wenye afya.
Jaribio la uvumilivu – Sparta
Katika simulizi za kale za Sparta, bwana harusi alipimwa uvumilivu kwa kupigwa fimbo au mawe kama ishara ya uthabiti wa maisha ya ndoa.
Kutoka Ulaya hadi Asia, Afrika hadi Mashariki ya Mbali, mila hizi zinaonyesha namna ndoa ilivyo zaidi ya sherehe—ni mkataba wa kijamii, kiroho na kitamaduni. Ingawa baadhi ya desturi hizi zinaweza kuonekana za ajabu kwa macho ya leo, kwa jamii husika ni hazina ya utambulisho na urithi wao.
Je, wewe ungeweza kushiriki katika mila ipi kati ya hizi?
