Kwa zaidi ya karne 14, nafasi ya juu ya kiroho katika Kanisa la Anglikana la Canterbury, limekuwa likishikiliwa na wanaume pekee, lakini mwaka 2026 historia hiyo ilipata sura mpya baada ya Sarah Mullally kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuongoza kanisa hilo lenye waumini zaidi ya milioni 80 duniani.
Uteuzi wake haukuonekana tu kama tukio la kawaida la kiutawala katika kanisa, bali kama ishara ya mabadiliko makubwa ya kijamii na kidini kuhusu nafasi ya wanawake katika uongozi wa taasisi za kidini.
Safari yake kufikia kilele hicho ni hadithi ya kuvutia ya mwanamke aliyeanza maisha kama muuguzi hospitalini, baadaye akafuata wito wa kiroho na hatimaye kuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika ulimwengu wa Ukristo.
Mwanzo wa maisha na ndoto za utumishi
Sarah Elisabeth Bowser alizaliwa Machi 26, 1962, katika mji wa Woking, nchini United Kingdom. Alikulia katika familia ya kawaida yenye watoto wanne, na tangu akiwa mdogo alionesha tabia ya kuwajali wengine.
Ndoto yake ya awali ilikuwa kufanya kazi inayogusa maisha ya watu moja kwa moja. Hivyo, aliamua kusomea uuguzi katika chuo cha London South Bank Polytechnic na kufanya mafunzo katika Hospitali ya St Thomas’ jijini London.
Mwaka 1984 alihitimu na shahada ya Sayansi ya Uuguzi. Baadaye alipata shahada ya uzamili katika masuala ya afya ya jamii, akijikita katika uongozi wa huduma za afya.
Katika miaka hiyo ya mwanzo ya kazi, Mullally alijijengea sifa ya kuwa muuguzi mwenye nidhamu, anayewajali wagonjwa na mwenye uwezo wa kuongoza timu.
Umahiri wake ulimfikisha katika nafasi ya juu serikalini. Mwaka 1999 aliteuliwa kuwa muuguzi mkuu wa Uingereza, nafasi ya juu kabisa kwa wauguzi nchini humo.
Katika wadhifa huo alisimamia sera za kitaifa za uuguzi na huduma za afya katika Mfumo wa Taifa wa Huduma za Afya.
Kipindi chake cha uongozi kilijulikana kwa juhudi za kuboresha hadhi ya taaluma ya uuguzi, kuboresha mazingira ya kazi kwa wauguzi na kusisitiza ubora wa huduma kwa wagonjwa.
Kwa mchango huo, mwaka 2005 alitunukiwa heshima ya kitaifa ya Dame Commander of the Order of the British Empire (DBE), mojawapo ya tuzo kubwa zinazotolewa na serikali ya Uingereza.
Lakini wakati taaluma yake ya afya ikiendelea kung’ara, ndani yake kulikuwa na wito mwingine uliokuwa ukimvuta huduma ya kiroho.
Miaka ya 2000, Mullally alianza kuhisi wito wa kuingia katika huduma ya kanisa. Uamuzi huo haukuwa rahisi, kwani ulimlazimu kuacha kazi yenye hadhi kubwa serikalini.
Mwaka 2001 aliwekwa wakfu kuwa shemasi katika Kanisa la Uingereza, na mwaka uliofuata akawa kasisi.
Hatimaye, mwaka 2004 aliacha kazi yake serikalini ili kujikita kikamilifu katika huduma ya kanisa.
Katika mahojiano mbalimbali baadaye alisema kuwa huo ulikuwa uamuzi mkubwa zaidi katika maisha yake.
“Nilijua kuna wito wa kuhudumia watu kwa njia tofauti,” aliwahi kusema.
Huduma yake ndani ya kanisa ilianza kuvutia macho ya viongozi wakuu wa taasisi hiyo.
Mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Canon Treasurer wa Kanisa Kuu la Salisbury, moja ya makanisa ya kihistoria nchini Uingereza.
Miaka mitatu baadaye, 2015, aliteuliwa kuwa Askofu wa Crediton, hatua iliyomfanya kuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kuwa maaskofu katika Kanisa la Uingereza.
Uteuzi huo ulitokea muda mfupi baada ya kanisa hilo kuruhusu wanawake kushika nafasi ya uaskofu, uamuzi uliokuwa umejadiliwa kwa miaka mingi.
Mwaka 2018 Mullally aliandika historia nyingine alipoteuliwa kuwa Askofu wa London, mojawapo ya nafasi tatu za juu zaidi katika uongozi wa kanisa.
Jimbo la London ni moja ya majimbo makubwa na yenye ushawishi mkubwa katika Kanisa la Uingereza. Katika nafasi hiyo alisimamia makanisa mengi pamoja na miradi ya kijamii inayolenga kusaidia maskini, wahamiaji na watu wasio na makazi.
Ajiandikia historia Canterbury
Mwaka 2026 Mullally aliandika historia kubwa zaidi baada ya kuthibitishwa kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury.
Nafasi hiyo inamfanya kuwa kiongozi wa kiroho wa Kanisa la Anglikana duniani na mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi katika Ukristo.
Pia ni mmoja wa maaskofu wanaoketi katika Baraza la Mabwana la Bunge la Uingereza, taasisi inayoshiriki katika mchakato wa kutunga sheria nchini humo.
Katika hotuba yake ya kwanza baada ya uteuzi huo, Mullally alisisitiza umuhimu wa haki, uwazi na upatanisho ndani ya kanisa.
Alisema kanisa linapaswa kuwa mahali pa matumaini na huruma kwa watu wote bila ubaguzi.
Pamoja na mafanikio hayo ya kihistoria, Mullally anarithi uongozi katika kipindi chenye changamoto.
Kanisa la Anglikana linakabiliwa na kupungua kwa idadi ya waumini katika baadhi ya nchi za Ulaya, migogoro kuhusu masuala ya kijamii kama ndoa za jinsia moja, pamoja na shinikizo la kurejesha imani ya jamii baada ya kashfa za unyanyasaji zilizowahi kulikumba kanisa.
Wachambuzi wanaamini uteuzi wa Mullally ni jaribio la kanisa kupata kiongozi mwenye uwezo wa kuleta maelewano katika kipindi hiki kigumu.
Mtaalamu wa masuala ya dini katika Chuo Kikuu cha Durham, Profesa Linda Woodhead, aliwahi kueleza kuwa Mullally ana sifa ya kuwa kiongozi “anayesikiliza na anayeweza kuunganisha makundi tofauti ndani ya kanisa.”
Mbali na majukumu yake ya kiroho, Mullally ni mke na mama wa watoto wawili. Aliolewa na Eamonn Mullally mwaka 1987.
Anasema mara nyingi kuwa uzoefu wake kama muuguzi ulimfundisha umuhimu wa huruma na kusikiliza watu, maadili ambayo ameyabeba katika uongozi wake wa kanisa.
Kwa wanaomfahamu, Mullally anaonekana kuwa kiongozi mwenye utulivu, unyenyekevu na mtazamo wa huduma kwa jamii.
Ishara ya mabadiliko katika taasisi za dini
Kwa wanawake wengi duniani, safari ya Sarah Mullally imekuwa ishara ya kuvunjika kwa vikwazo vilivyodumu kwa karne nyingi katika taasisi za kidini.
Kutoka hospitalini hadi madhabahuni, kutoka muuguzi hadi Askofu Mkuu wa Canterbury, maisha yake yanaonesha jinsi uongozi unaweza kubadilika na kufungua milango kwa kizazi kipya cha wanawake katika dini.
Akiwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu katika Kanisa la Anglikana, Mullally anabeba matumaini ya wengi wanaoamini kuwa taasisi za kidini zinaweza kubadilika na kuendana na wakati bila kupoteza misingi yake ya kiroho.
Na wakati dunia ikiangalia hatua zake za kwanza katika uongozi huo, jambo moja linaonekana wazi: ukurasa mpya umefunguliwa katika historia ya kanisa hilo.
Imeandikwa na Elizabeth Edward kwa msaada wa mitandao.
