Mbeya. Serikali imesema itaendelea kushirikiana na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ili kuhakikisha fursa zinazojitokeza kiuchumi na kijamii zinawanufaisha vijana na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo Machi 29,2026 wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Biashara Kadinda, Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa, amesema Serikali inathamini mchango wa wawekezaji katika maendeleo ya uchumi wa nchi. Amesema kushirikiana nao na kuwawekea mazingira mazuri kutasaidia kuendeleza fursa zinazozalisha ajira na kuongeza maendeleo kwa wananchi.
Meya Issa amebainisha kuwa Jiji la Mbeya limeonesha mabadiliko kutokana na uwekezaji unaojitokeza, hali inayochochea uchumi na kufungua milango zaidi ya ajira. “Nikuhakikishie mwekezaji, uko sehemu sahihi na Serikali itashirikiana nawe kuhakikisha unafikia malengo yako, kwani uwekezaji huu si tu faida kwako, bali pia vijana na halmashauri tutanufaika.”
Mwekezaji, Dickson Kadinda amesema uwekezaji huo uliogharimu zaidi ya Sh200 milioni umetoa ajira 28 za moja kwa moja na mpango ni kuongeza kuwa zaidi ya 58. Kadinda ameeleza kuwa sapoti ya Serikali na mikopo yenye riba nafuu imesaidia kufanikisha mradi huo licha ya changamoto.
Diwani wa Kata ya Ruanda, Isack Mwakubombaki, amesema matarajio ni kuona kituo hicho kikizalisha ajira nyingi na kuongeza pato la kata na Taifa kwa ujumla. Mmoja wa wadau wa maendeleo, Ibrahim Mbembela ‘Maziwa,’ amesema sekta binafsi imetoa mchango mkubwa katika kuunda ajira na kuondoa vijana katika mazingira hatarishi.
