KOCHA Mkuu wa Mafunzo, Salum Ali Haji, amesema sababu ya kupoteza mchezo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) raundi ya 21 dhidi ya KVZ ni wachezaji wake kuumwa na tumbo la kuharisha.
Kauli hiyo imekuja baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa KVZ katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar iliyochezwa jana Jumamosi Machi 28, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja.
Amesema, isivyo bahati wachezaji wa timu hiyo walipata changamoto kuanzia kambini kwani hawakujua chakula kimewekwa kitu gani, hivyo jambo hilo limesababisha kucheza chini wangu.
“Hatujui chakula kimepata changamoto gani maana wachezaji walikuwa wanacheza huku wanaharisha, hivyo hilo limesababisha wachezaji wetu kucheza chini kiwango,” amesema.
Amesema kupitia changamoto hiyo, wamejifunza na kuahidi kuwa makini isijitokeze tena kwa mechi zijazo.
Amesema, mechi hiyo haikuwa nzuri upande wao ila amewapongeza KVZ kwa ushindi huo.
Kipigo hicho kimeifanya Mafunzo kuendelea kusalia nafasi ya kumi katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na alama 27, huku KVZ ikipanda kileleni ikifikisha alama 40.
