Bibi afungwa jela miaka 30 baada ya kukutwa na bangi

Mtwara. Mahakama ya Wilaya ya Mtwara imemuhukumu Hawa Ally (60) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki dawa za kulevya aina ya bangi.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 27, 2026  na Hakimu Mkazi Mfawidhi, George Mbago, aliyesikiliza kesi hiyo.

Kwa mujibu wa mashtaka, mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 28, 2025 katika mtaa wa Bomba la Bure, Kata ya Magomeni mkoani Mtwara, ambapo alikutwa na bangi yenye uzito wa gramu 90.

Akisoma hukumu, Hakimu Mbago alisema kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 16(1) na 2(c) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 (marejeo ya 2023).

Awali, mshtakiwa alikana shtaka hilo aliposomewa kwa lugha anayoielewa, hali iliyosababisha upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi ili kuthibitisha kesi bila kuacha shaka.

Katika kuimarisha hoja zao, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita pamoja na vielelezo saba.

Mahakama yasikiliza ushahidi

Shahidi wa pili, Venance Lukondya, alieleza kuwa Agosti 27, 2025 walipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kuhusu uwepo wa mshtakiwa anayejihusisha na uuzaji wa bangi katika eneo la Bomba la Bure.

Alisema siku iliyofuata saa sita usiku, yeye pamoja na maofisa wengine walifika nyumbani kwa mshtakiwa wakiongozana na mjumbe wa serikali ya mtaa na kufanya upekuzi kwa ridhaa yake.

Katika upekuzi huo, walikuta kifurushi cha bangi kikiwa kimehifadhiwa ndani ya mfuko wa kijani maarufu kama ‘mfuko wa Magufuli’ nyuma ya nyumba.

Aliongeza kuwa baada ya kugunduliwa, mshtakiwa alikiri kuwa ni bangi na kudai huitumia kama dawa ya asili.

Kielelezo hicho kilikamatwa na taratibu za kisheria kufuatwa kabla ya kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.

Shahidi wa kwanza, Abdillahi Mustafa kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, alithibitisha kuwa baada ya uchunguzi, majani hayo yalibainika kuwa bangi yenye uzito wa gramu 90, mojawapo ya dawa za kulevya zilizopigwa marufuku kisheria.

Kwa upande wake, shahidi wa tatu Ajiri Omary ambaye ni mjumbe wa serikali ya mtaa, alisema alishuhudia upekuzi huo baada ya kuchukuliwa na polisi kama shahidi, ambapo aliona mfuko wenye majani yanayodhaniwa kuwa bangi ukipatikana nyuma ya nyumba ya mshtakiwa.

Mashahidi wengine wa upande wa mashtaka, wakiwemo askari polisi, walieleza namna operesheni ya ukamataji ilivyofanyika huku wakisisitiza kuwa taratibu zote zilifuatwa.

Aidha, shahidi Abdallah Salumu Chilambo, ambaye ni kaka wa mshtakiwa alidai mahakamani kuwa mshtakiwa alikiri kupatikana na bangi wakati wa kuandika maelezo yake polisi, mbele yake.

Mshtakiwa adai kubambikizwa kesi

Katika utetezi wake, mshtakiwa alidai kubambikizwa kesi hiyo na askari polisi, akisema hawakukuta kitu ndani ya nyumba yake bali walidai kuona kifurushi hicho nje ya nyumba.

Alieleza pia kuwa alilazimishwa kusaini nyaraka za ukamataji na kutoa maelezo ya kukiri kosa kutokana na hofu aliyokuwa nayo.

Mshtakiwa alisisitiza kuwa hajawahi kujihusisha na biashara ya bangi wala matumizi ya dawa hizo, akiomba mahakama izingatie utetezi wake.

Baada ya kusikiliza pande zote, mahakama ilieleza kuwa upande wa mashtaka umefanikiwa kuthibitisha kesi bila kuacha shaka yoyote ya msingi.

Kutokana na hilo, mshtakiwa alipatikana na hatia ya kumiliki dawa za kulevya kinyume cha sheria na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani.

“Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka umefanikiwa kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka yoyote ya msingi, hivyo mshtakiwa amepatikana na hatia na mahakama inamuhukumu kwenda gerezani miaka 30”. Alieleza Hakimu

Aidha, mahakama ilitoa amri ya kuteketezwa kwa gramu 90 za bangi iliyokamatwa chini ya usimamizi wa Polisi na Mahakama.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, mshtakiwa aliomba kupunguziwa kifungo akidai kuwa ni tegemezi kwa mama na bibi yake kipofu, pamoja na kusumbuliwa na maradhi ya moyo na miguu.