KITENDO cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kufungwa bao 1-0 dhidi ya Liechtenstein, kimewaibua wadau ambao walikuwa na mitazamo tofauti ya nini kifanyike ili kupata matokeo mazuri.
Alhamisi ya Machi 26, 2026, Taifa Stars ilipoteza mechi hiyo katika mashindano ya FIFA Series yanayofanyika Kigali huko Rwanda ambapo leo Jumapili itacheza mechi nyingine dhidi ya Macau kwenye Uwanja wa Pele nchini humo.
Kabla ya kipigo hicho, Taifa Stars ilifungwa 1-0 na Morocco katika hatua ya 16 bora ya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika(AFCON 2025) ambapo pia hatua ya makundi ilifungwa 2-1 na Nigeria, kisha ikatoka sare ya 1-1 dhidi ya Uganda na Tunisia. Matokeo hayo kwa ujumla, yameishusha Tanzania nafasi tatu katika viwango vya FIFA kutoka 110 hadi 113.
Kutokana na mwenendo huo, wapo waliyoiunga mkono kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda aliyoitoa kwa kocha Miguel Gamondi kupewa muda wa kuitengeneza timu ndani ya miaka miwili aliyosaini.
Miongoni mwa hao ni kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyesema inahitaji uvumilivu ili kumpa kocha muda wa kutengeneza timu kwa malengo mapana ya baadaye.
“Wenzetu nje kabla ya ligi zao kuisha wanakuwa wanaendelea na programu za timu za taifa, tofauti na hapa kwetu, hivyo mafanikio hayawezi kuja kwa haraka bila kuweka misingi imara, kikubwa kocha Gamondi alipewa uhuru na Waziri Makonda kutengeneza timu, naamini atafanya hivyo,” alisema Dida na kuongeza:
“Nakumbuka aliyekuwa kocha wa timu za taifa za Tanzania, Kim Poulsen alipewa jukumu la kutengeneza timu ya vijana wa Serengeti Boys wa mwaka 2017, walifanya vizuri na wengi wao wanacheza timu mbalimbali za Ligi Kuu kama Dickson Job, Nickson Kibabage, Kibwana Shomari na wengine lakini ile ilikuwa programu ya muda mrefu hakikuwa kitu cha kuibuka timu na sasa wachezaji hao ni muhimu katika timu ya taifa ya wakubwa.”
Kipa aliyewahi kuichezea Geita Gold, Kelvin Kayego ni kati ya vijana waliowahi kuandaliwa na kocha Poulsen kwa muda mrefu, alisema: “Kusema ukweli timu ikikaa kwa pamoja muda mrefu, kunakuwa na mafanikio makubwa, tofauti na kukutana kwa muda mfupi, ndiyo maana Serengeti Boys ya 2017 ilikuwa ya moto, tulikaa kwa pamoja kwa miaka miwili ambapo kocha alikuwa anatufuatilia kuanzia uwanjani hadi maisha yetu ya kila siku.”
Mwingine aliyechangia nini kifanyike ili Stars iweze kupata matokeo ya ushindi ni kipa Mohamed Said ‘Nduda’ aliyewahi kuzichezea Simba, Yanga na Stars, alisema: “Kama kocha amepewa muda wa miaka miwili ya kutengeneza timu, inahitajika subra na utulivu ili baadaye ije ipatikane timu itakayofanya makubwa, hilo linawezekana kwa kuzingatia misingi sahihi na siyo kutaka mafanikio ya haraka, ingawa kwa wachezaji wanaopata nafasi ya kuitwa Stars waonyeshe kupambana kwa bidii.”
Beki wa zamani wa Yanga na Stars, William Mtendamema, alisema: “Pamoja na kocha kupewa muda mrefu wa kuandaa timu, wachezaji wajitume na kupambania taifa lao na kuona fursa hiyo inapandisha CV zao, maana kuna timu za nje zikiwataka zitataka kuangalia kama mchezaji anaichezea timu ya taifa lake, hiyo ni heshima kubwa.”
Kocha wa zamani wa Stand United ‘Chama la Wana’, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema: “Kiuchezaji timu haipo vibaya, nadhani huu ndiyo muda sahihi ambao kocha anaangalia kitu gani kifanyike ili kuandaa Stars itakayokuwa na mafanikio makubwa ya baadaye.”