Aliyemuua mwanamke na kumkata sehemu za siri akwaa kisiki Mahakama ya Rufaa

Arusha. Mahakama ya Rufaa imebariki hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyekuwa amehukumiwa Mulabu Muya baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Nyabise Webiro kwa kumkata sehemu zake za siri na kuondoka nazo.

Hata hivyo, mrufani wa kwanza, Mgwasi Wapori, ameachiwa huru baada ya mahakama kuridhika kuwa ushahidi dhidi yake haukuthibitisha kosa.

Tukio hilo lilitokea Septemba 25, 2022, katika Kijiji cha Nyegina, Wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Nyabise Webiro alikutwa akiwa katika dimbwi la damu na ndugu zake, akiwa na majeraha makubwa, ikiwemo sehemu zake za siri kukatwa.

Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa umetolewa Machi 26, 2026, na jopo la majaji watatu, Dk Gerald Ndika, Patricia Fikirini na Mustafa Ismail, waliokuwa wakisikiliza rufaa ya jinai namba 699/2023.

Jaji Ismail alisema mahakama iliridhika ushahidi dhidi ya mrufani wa pili ulithibitisha kosa, ikiwemo ungamo lake alioutoa kwa hiari, likiashiria mpango wa kutekeleza mauaji, silaha iliyotumika na majeraha aliyosababishiwa marehemu.

Awali, Mahakama Kuu ilidai kuwa usiku wa tukio Nyabise alikumbana na mashambulizi makali nyumbani kwake. Binti yake na kaka yake walithibitisha kuwa akiwa kwenye maumivu kabla ya kufariki (Nyabise Webiro) aliwaleza kuwa alishambuliwa na warufani hao waliomkata sehemu zake za siri.

Marehemu alipelekwa Hospitali ya Nyasho, na baadaye Rufaa ya Musoma, lakini alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi na majeraha makubwa. Uchunguzi wa kitabibu ulithibitisha kuwa marehemu alibakwa na kuwa na majeraha makubwa kichwani, tumboni na sehemu zake za siri.

Warufani wote wawili walikutwa na hatia ya mauaji, huku hukumu ya kunyongwa hadi kufa ikitokana na ushahidi wa maelezo ya marehemu na ya mrufani wa pili. Hata hivyo, rufaa ilitolewa wakipinga uhalali wa ushahidi na ushahidi wa kukiri kosa.

Baada ya kupitia hoja za pande zote, Mahakama ya Rufaa iliridhika ushahidi wa mrufani wa pili ulikuwa wa kutosha kuthibitisha kosa bila shaka, lakini ushahidi wa mrufani wa kwanza haukutosha, hivyo kuamuru aachiwe huru.

Jaji Ismail alibainisha kuwa tamko la kifo ni aina ya ushahidi unaokubalika kisheria endapo litatolewa kwa hiari na katika hali ya utimamu wa akili. Katika kesi hii, tamko la mrufani wa pili lilithibitisha mpango wa mauaji na hali ya tukio, huku likiungwa mkono na ushahidi wa kitabibu.

Mahakama ilihitimisha kuwa hukumu ya mrufani wa pili ilithibitishwa bila shaka, huku upande wa mashtaka ukithibitisha kosa hilo kikamilifu.