Nchimbi Amwakilisha Rais Samia Katika Mkutano wa OACPS Guinea ya Ikweta

Global Publishers
March 29, 2026
0 Comments

Makamu wa Rais Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, akimwakilisha Rais Dkt. Samia katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Sipopo kilichopo Jijini Malabo nchini Guinea ya Ikweta.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Sipopo kilichopo Jijini Malabo nchini Guinea ya Ikweta.

Katika ufunguzi wa Mkutano huo, salamu za Viongozi mbalimbali zimesisitiza umuhimu wa hitaji la kufanya mageuzi ya Kitaasisi na kimfumo kuwezesha Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia kwa sasa ikiwemo, migogoro ya kisiasa, vita pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Vilevile, Ufunguzi wa Mkutano huo, umeweka mkazo kwa nchi wanachama kutoa michango kwa wakati ili kuifanya Taasisi ya OACPS kujitegemea kifedha na kuwa sauti huru kwenye jumuiya ya kimataifa. Pia msisitizo umewekwa katika kutumia vema rasilimali watu ambao ni bilioni 1.5 waliopo katika jumuiya hiyo kwa kuwajengea uwezo, ubunifu na matumizi ya akili unde ili kuleta maendeleo.

Halikadhalika, Mkutano huo umesisitiza umuhimu wa kukuza biashara baina ya nchi wanachama pamoja na jumuiya zingine za kikanda. Pia kuwajengea uwezo vijana na wanawake ili waweze kushiriki vema katika shughuli za maendeleo.

Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za kuendelea kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, na kudhihirisha mchango wa nchi katika mijadala ya maendeleo na ushirikiano wa kimataifa.

Katika Mkutano huo, Rais wa Angola, Mhe. Joao Manuel Lourenzo, amekabidhi Uenyekiti wa Jumuiya ya OACPS kwa Rais wa Guinea ya Ikweta Mhe. Teodoro Obiang Nguema Mbasogo.