BAADA ya kukaa nje kwa takribani mwezi mzima, kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Nassor Saadun, ameanza kufanya mazoezi na wenzake, ikiwa ni matumaini mapya pia kwa kikosi hicho kutokana na mechi mbili ngumu zijazo za Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Azam, Mbaruku Mlinga, alisema nyota huyo alipata majeraha ya nyama za paja ndio maana alikosekana uwanjani kwa muda mrefu, ingawa baada ya programu binafsi kwa sasa amejumuika na wachezaji wenzake.
“Awali alikuwa chini ya uangalizi wa jopo la madaktari kutokana na majeraha yaliyokuwa yanamkabili, ila kwa sasa tayari tumemruhusu kuungana na wenzake, naamini hadi Ligi Kuu Bara itakaporejea atakuwa fiti kwa asilimia 100,” alisema Mlinga.
Mlinga, alisema suala la kucheza nyota huyo mechi zijazo itategemea na mapendekezo ya benchi la ufundi, ingawa kuungana na wenzake mazoezini ni ishara tosha yupo fiti kucheza, akiongeza upana wa machaguo kutokana na umuhimu wake kikosini.
Urejeo wa nyota huyo unaongeza morali kwa kikosi cha Azam, chini ya Kocha Mkongomani, Florent Ibenge, kutokana na ratiba ngumu ya ligi, ambapo Aprili 1, 2026, itacheza dhidi ya Singida Black Stars, kisha Aprili 5, 2026, itaikabili Simba.
Majeraha ya mara kwa mara yanayomsumbua Saadun, yamemfanya mchezaji huyo kufunga bao moja tu Ligi Kuu Bara msimu huu, ambalo ni la ushindi kwa Azam wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, Septemba 24, 2025.
Msimu uliopita wa 2024-2025, nyota huyo alifunga mabao manane ya Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho cha Azam, akishika nafasi ya pili kwa nyota wazawa waliofunga mabao mengi, nyuma ya Clement Mzize wa Yanga aliyefunga 14.
Mabao manane aliyoyafunga Saadun, yalikuwa ni sawa na yaliyofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Paul Peter Kasunda, ambaye kwa sasa anaichezea JKT Tanzania, huku akiwa tayari msimu huu ameifungia mabao matano.
