Mgaboni TRA United afichua jambo Ligi Kuu Bara

KIPA wa TRA United raia wa Gabon, Jean-Noel Amonome, amesema msimu huu umekuwa mzuri kwake na rahisi wa kusoma vizuri mazingira ya Ligi ya Tanzania, tofauti na mwanzo alipojiunga na kikosi hicho, ambapo alihitaji kupewa muda zaidi kuzoea.

Nyota huyo aliyejiunga na TRA United zamani Tabora United, Januari 3, 2025, akitokea AS Arta/Solar7 ya Djibouti, alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja aliocheza Ligi Kuu Bara kuna vitu vingi amejifunza, ambavyo vimekuza pia karia yake.

“Unapotoka Ligi moja kwenda nyingine halafu ukawa unapewa kipaumbele zaidi unapaswa kupambana sana, wakati nasajiliwa kwa bahati nzuri nina marafiki wengi wanaocheza Tanzania, hivyo haikuwa ngumu kwa sababu walinisaidia,” alisema Amonome.

Kipa huyo aliyewahi kucheza FC 105 Libreville ya kwao Gabon, AmaZulu FC, Royal Eagles na Uthongathi FC zote za Afrika Kusini, alisema kwa sasa anafurahia maisha ya Tanzania, kutokana na ushindani wa Ligi ambao unamfanya azidi kupambana.

“Kama timu tuko katika mwelekeo mzuri kwa sababu tuna wachezaji na benchi la ufundi bora, ushindani msimu huu ni mkubwa sana kutokana na mahitaji ya kila mmoja wetu, sisi tutaendelea kupambana ikiwezekana tumalize hata nafasi nne za juu.”

Katika msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na kikosi hicho Januari 3, 2025, Amonome alimaliza na ‘Clean Sheets’ mbili za Ligi Kuu Bara, ingawa kwa msimu huu wa 2025-2026, tayari ana sita, akipitwa nne tu na kinara Djigui Diarra wa Yanga mwenye 10.