Dar es Salaam. Katika mjadala ulioandaliwa na Shirika la Msichana Initiative jijini Dar es Salaam jana Machi 28, 2026, viongozi wa dini wameeleza kuwa elimu ndiyo silaha muhimu zaidi ya kupambana na ndoa za utotoni.
Walisema pia kuna haja ya sheria kuweka misingi imara itakayozuia watoto kuingia kwenye ndoa kabla ya kuendelea kimaisha. Wakizungumza katika mjadala huo, viongozi wa dini walisema mafundisho ya dini hayaungi mkono ndoa za utotoni, bali yanahimiza ulinzi, elimu na ukomavu wa watoto kabla ya kuanza maisha ya ndoa.
Baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki mjadala kuhusu ndoa za utotoni uliondaliwa na Shirika la Msichana Initiative.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka, alibainisha kuwa bado kuna mianya ya kisheria inayoruhusu ndoa za utotoni, jambo linalohitaji marekebisho ili kulinda haki za mtoto.
Kwa sasa, mtoto wa kike anaweza kuolewa akiwa na miaka 14–15 kwa idhini ya wazazi au mahakama, hali inayochochea ndoa za utotoni katika baadhi ya maeneo. Sheikh Mataka alisema ni muhimu kuhakikisha mtoto anamaliza elimu ya sekondari akiwa na umri wa 18, sambamba na kubadilisha mitazamo ya jamii kuhusu ndoa za mapema. Aliendelea kufafanua kuwa mafundisho ya dini ya Kiislamu yanasisitiza umuhimu wa ukomavu kabla ya kuingia ndoa na kuangalia kwanza masilahi ya mtoto.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Sheikh Khamis Mataka akizungumza wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini kujadili suala la ndoa za utotoni.
Kwa upande wake, Padri Longino Rutagwelera kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania alisema kuwa katika mtazamo wa Kikristo, ndoa ni taasisi takatifu inayopaswa kuhusisha watu waliokomaa na wenye uelewa wa majukumu ya kifamilia. Ndoa inapaswa kufungwa kwa hiari ya wahusika na si kwa kulazimishwa. Padri Rutagwelera alisisitiza kuwa mtu anapaswa kuingia kwenye ndoa akiwa na uwezo wa kufikiri kwa uhuru, kufanya maamuzi sahihi na kubeba majukumu ya kifamilia.
Wakili Lucy Gidamis kutoka Msichana Initiative aliomba Serikali na Bunge kufanya marekebisho ya vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ili kuweka umri wa chini wa kuoa na kuolewa kuwa miaka 18, kulinda haki za watoto na kuendana na mikataba ya kimataifa ya haki za mtoto.
Baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki mjadala kuhusu ndoa za utotoni uliondaliwa na Shirika la Msichana Initiative.
Alisema ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini, Serikali, mashirika ya kiraia na jamii, ni muhimu kufanikisha juhudi za kupinga ndoa za utotoni na kubadilisha mitazamo isiyo salama ya kijamii. Alisema mafanikio ya kupinga ndoa za utotoni yataegemea sauti ya pamoja ya wadau na jitihada za pamoja katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za elimu na ustawi.

