MSHAMBULIAJI wa Al Nassr ya Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia, Clara Luvanga amefikia rekodi yake ya msimu uliopita ya kufunga mabao 21 kukiwa bado mechi mbili za kumaliza mashindano hayo.
Clara alifunga mabao matatu kwenye mechi ya dabi dhidi ya Al Hilal walipoondoka na ushindi wa mabao 4-1 yaliyomfanya afikishe idadi ya mabao 21 akiwa anaongoza kwa ufungaji bora.
Mabao aliyofunga nyota huyo wa zamani wa Yanga Princess yamefanya Al Nassr kutangazwa mabingwa ikiwa bado ina mechi mbili mkononi.
Al Nassr imefikisha pointi 33 kwenye mechi 12 ilizocheza huku Al Ittihad ikiwa nafasi ya pili ikikusanya pointi 25 ambazo hata ikishinda mechi mbili zilizosalia haiwezi kuzifikia.
Kwa ujumla Clara ana nafasi kubwa ya kutwaa kiatu cha mfungaji bora wa ligi msimu huu kutokana na nafasi kubwa aliyowaacha wanaomkimbiza kwenye mbio hizo.
Anayefuata ni Adriana Silva wa Al Qadsiah mwenye mabao 13 mwingine ni Lea Le Garrec mwenye nayo 11 na wote wawili wamebakiza mechi mbili za kumaliza ligi.
Hivyo kama Clara ataendelea kucheza mechi zilizosalia na kufunga anaweza kuondoka na kiatu alichokipigania ndani ya misimu mitatu mfululizo tangu alipojiunga na chama hilo akitokea Dux Lugrono ya Hispania.
