Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watuhumiwa wanane kwa tuhuma za kuhusika na matukio matatu tofauti ya uhalifu, likiwemo la mauaji ya mwanamke na mtoto wake mchanga waliotumbukizwa kisimani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema hayo leo Jumapili Machi 29, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari, akieleza kuwa hatua hiyo imetokana na operesheni maalumu iliyofanyika katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, tukio kubwa zaidi linamhusu Mwajabu Shaban (30) pamoja na mtoto wake wa miezi minne, Mwantumu Abdala, waliouawa Machi 28, 2026 saa tisa alasiri katika Kitongoji cha Tawini kwa Mgongo, Kijiji cha Kisangasa, Wilaya ya Kilindi.
Amesema baada ya mauaji hayo, miili ya marehemu ilitumbukizwa ndani ya kisima cha maji.
“Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wanaohusishwa na tukio hili ambao ni Kilo Msami, Abdallah Ibrahim, Hamis Ayub na Bigfai Edward, na uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha tukio hilo,” amesema Muchunguzi.
Katika tukio lingine, watu wawili, Sharing Mustafa, maarufu Charada na Adamu Hassani, maarufu Masozy, wanashikiliwa kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili, Yassin Amiri, fundi simu mkazi wa Makorora jijini Tanga.
Aidha, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili, Shani Gugu mkazi wa Kange jijini Tanga na Bakari Hamza mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia 16 ambazo zingekuwa halali zingekuwa na thamani ya Sh160,000.
“Watuhumiwa hawa walikuwa wakichanganya noti hizo bandia na fedha halali kwa lengo la kujipatia bidhaa na huduma mbalimbali,” ameeleza kamanda huyo.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limetoa taarifa ya tukio la mlipuko wa petroli uliotokea Machi 28, 2026 saa 12:30 jioni katika Kijiji cha Bongi, Kata ya Sindeni, Wilaya ya Handeni, uliosababisha kifo cha mtoto aitwaye Nilham Ramadhani (8).
Watu wengine watatu, Murtaza Abdallah, Latifa Michael na Shafii Abdallah, walijeruhiwa katika tukio hilo na wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.
Sambamba na hilo, katika msako unaoendelea dhidi ya matumizi ya vyombo vya moto visivyo na usajili, Jeshi la Polisi limekamata pikipiki 11 zisizo na namba za usajili..
Kamanda Muchunguzi amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini uhalali wa pikipiki hizo pamoja na sababu za kutokuwa na namba za usajili, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa kulingana na ushahidi utakao patikana.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya uhalifu na kuwahakikishia wananchi usalama wao.
