Kigoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ameibua hoja mahakamani katika shauri la uchaguzi la kupinga ushindi wa mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando au Baba Levo (CCM), kuhusiana na dhamana ya gharama za uchaguzi.
Hoja hiyo ni uhalali wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kutoa msaada wa kisheria bure kwa walalamikaji ambao ni Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, akisema TLS haina mamlaka ya kutoa msaada huo.
Walalamikaji wanawakilishwa na wakili John Seka, aliyeteuliwa na TLS kuwawakilisha kortini, lakini AG ameibua hoja inayogusa uhalali wa kisheria wa TLS kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo.
AG, kupitia kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Marko Mulwambo, amewasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kusajili maombi ya mapitio dhidi ya uamuzi wa kukataa pingamizi lao, uliotolewa na Mahakama Kuu Kigoma, Desemba 16, 2025.
Mlalamikiwa wa kwanza ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na wa tatu ambaye ni AG, waliwasilisha mapingamizi mawili dhidi ya shauri hilo lilipofunguliwa, na moja ilihusu dhamana ya gharama za shauri la uchaguzi.
Kwamba, Mahakama haikuwa na mamlaka ya kupanga tarehe ya kusikiliza shauri hilo la uchaguzi kwa kuwa dhamana ya gharama haijaombwa na haijalipwa, kinyume na Kifungu cha 140(2), (3), (5) na (7) cha Sheria ya Uchaguzi ya 2024.
AG aliomba shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kigoma Mjini lifutwe, akisisitiza kwamba mchakato wa uombaji wa dhamana ya gharama za shauri la uchaguzi haujazingatiwa, licha ya wakili kuteuliwa na TLS.
Hata hivyo, Jaji Projestus Kayhoza alitupa pingamizi hilo na lingine walilokuwa wamewasilisha pamoja na mapingamizi matatu yaliyokuwa yamewasilishwa na mawakili wawili wa Baba Levo—Daniel Rumenyela na Emmanuel Msasa.
“Baada ya uchambuzi wote kuhusu mapingamizi ya awali ya kisheria yaliyowasilishwa na walalamikiwa, natamka kuwa mapingamizi hayo yote hayana nguvu ya kisheria na hayana mashiko, hivyo nayatupilia mbali,” alisema Jaji.
Katika maombi mapya yaliyowasilishwa kortini na AG Machi 2, 2026, na kutolewa uamuzi mdogo na Jaji Augustine Rwizile wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Machi 27, 2026, AG ameibua hoja mpya juu ya uhalali huo wa TLS.
Maombi hayo ni dhidi ya Johary Kabourou, Loum Mwita, Pendo Kombolela na Luma Akilimali kama mjibu maombi wa kwanza hadi wa nne, ambao ndio walalamikaji katika shauri la msingi, na Baba Levo kama mjibu maombi wa tano.
Katika uamuzi huo, Jaji Rwizile alirejea maombi mapya ya AG na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini, akisema wameomba kuongezewa muda wa kusajili maombi ya mapitio (review) juu ya uamuzi wa Desemba 16, 2025.
“Maombi hayo yaliletwa chini ya Kifungu cha 14(1) cha Sheria ya Ukomo wa Muda Sura ya 89, marejeo ya mwaka 2023, na Kifungu cha 105 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai Sura ya 33, marejeo ya mwaka 2023. Maombi yaliwasilishwa kwa hati ya dharura ikiambatanishwa na kiapo cha Wakili Mulwambo. Msingi wa maombi ni kwamba, wakati Mahakama ilitoa uamuzi, iliamini TLS kilikuwa na mamlaka ya kutoa msaada wa kisheria,” alieleza Jaji.
“Hata hivyo, wakaeleza kuwa baada ya kupata ufafanuzi rasmi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Februari 12, 2026, ilibainika kuwa usajili (cheti) wa TLS uliisha tarehe Aprili 28, 2022, hivyo haikuwa na uhalali kufanya hivyo mwaka 2025.”
Waombaji walijenga hoja kuwa taarifa hiyo ni ushahidi mpya ambao haukuwepo wakati wa kutolewa uamuzi husika, na kifungu cha 14(1) cha Sheria ya Ukomo kinahusu mamlaka ya mahakama kuongezea muda mashauri baada ya kikidhi vigezo.
Jaji alisema AG na msimamizi walijenga hoja kuwa kifungu hicho kinaeleza maombi ya kuongezewa muda ni utashi wa mahakama, ambao ni lazima utekelezwe kwa busara, kwa kuzingatia misingi ya haki na kanuni za kisheria, na si kiholela.
Jaji alisema waombaji waliendelea kueleza kwamba katika shauri hili, Mahakama ilitoa uamuzi Desemba 16, 2025, katika Shauri la Uchaguzi namba 28949 la 2025 kwa kuamini TLS kilikuwa na mamlaka halali ya kutoa msaada wa kisheria.
“Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, Desemba 12, 2025, waombaji walikuwa tayari wameanza kuchukua hatua za kutafuta uthibitisho rasmi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu uhalali wa mamlaka hayo (ya TLS),” alisema.
“Walieleza kuwa majibu kamili yalitolewa Februari 12, 2026, yakibainisha kuwa TLS haikuwa na usajili halali (wa kutoa msaada wa kisheria) kufikia Novemba 14, 2025. Baada ya kupata taarifa hiyo, waombaji waliwasilisha maombi haya.”
Jaji alisema waombaji walijenga hoja kuwa wamekidhi vigezo vyote vinavyotakiwa, kwa kuwa wameeleza kikamilifu sababu za kipindi chote cha ucheleweshaji, wameonesha kuwa ucheleweshaji wa siku 29 haukuwa wa kupita kiasi, na wameonesha bidii na umakini katika kufuatilia haki hiyo.
Jaji alisema katika majibu yao, mjibu maombi wa kwanza hadi nne, kupitia kwa wakili Seka, walieleza kuwa maombi hayo yanajaribu kuonesha uharamu ambao haukuonekana kwenye uso wa kumbukumbu.
Walieleza hoja ya TLS kutoa msaada wa kisheria haikuwepo mbele ya Mahakama ya awali na haiwezi kuhalalishwa kwa kuongezewa muda.
Kwa mujibu wa wakili Seka, kuongeza muda kwa hoja hiyo ni njia tu ya kutaka uamuzi tofauti kupitia uwani, na kwamba huo sio taratibu halali kisheria.
“Pia, wakili Seka alieleza kwamba ni sawa na kupanda farasi wawili (Riding Two Horses), na kuongeza kuwa Februari 2026, maombi haya yalifunguliwa mahakamani wakati tayari kuna Rufaa namba 87 ya mwaka 2026,” alisema Jaji.
Wakili Seka alisisitiza katika hoja yake kuwa taratibu wa kuendesha mashauri mawili yenye hoja sawa kwa wakati mmoja unakosa uhalali kisheria na unaitwa matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama au “kupanda farasi wawili.”
Jaji amemnukuu wakili Seka akisema: “Kukubali maombi haya, wakati Rufaa ikiendelea, ni kinyume na kanuni zilizowekwa na Mahakama ya Rufani.”
Wakili Seka aliendelea kusisitiza kwamba maombi hayo hayastahili, kwani yanahusisha hoja mpya, ambayo haiko kwenye uso wa rekodi, hivyo, njia sahihi ya hoja hizo ni kupitia rufaa, si kuongezwa muda wa kuwasilisha mapitio.
Jaji alisema kwa msingi huo, wakili aliomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi hayo, na kwamba waombaji hawaleti maombi ya gharama kwani ni wanufaika wa msaada wa kisheria walioupata kupitia TLS.
Kwa mujibu wa Jaji, mjibu maombi wa tano (Baba Levo), ambaye kimsingi ndiye mnufaika halisi wa maombi hayo, aliyaunga mkono.
Katika uamuzi wake, Jaji alisema baada ya kupitia kwa makini maombi hayo pamoja na viapo vya kuyaunga mkono, kiapo kinzani, na maelezo kutoka kwa pande zote, hoja ya msingi ni kama waombaji wanastahili kuongezewa muda.
“Nimepitia kumbukumbu za shauri la awali pamoja na mwenendo wake. Inaonekana wazi kuwa hoja bishaniwa ni suala la dhamana katika shauri la uchaguzi, kwa kuwa mtu aliyepewa msaada wa kisheria hatakiwi kulipia gharama za shauri wakati anafungua kupinga matokeo ya uchaguzi husika,” alisema Jaji.
“Nimeridhika kuwa waombaji wameonesha kwa kiwango kinachokubalika kisheria uwepo wa hoja ya kisheria na dhana ya kasoro za kiutaratibu zinazoonekana katika uamuzi wa Mahakama. Lakini, pia waombaji wametoa maelezo ya kuridhisha kuhusu sababu za ucheleweshaji wa kuwasilisha maombi haya. Kiapo chao kimeainisha sababu za ucheleweshaji kwa kila siku husika, kwa mujibu wa matakwa ya sheria,” alisema Jaji.
Kwenye uamuzi wake, alifafanua kuwa ucheleweshaji uliotokea haukutokana na uzembe, bali ulitokana na kusubiri uthibitisho rasmi wa kisheria kutoka kwa mamlaka husika, na baada ya kupata majibu walichukua hatua kuleta maombi mbele ya mahakama.
Alisema mahakama inakubaliana na hoja ya waombaji kuwa ucheleweshaji wao haukutokana na kuendesha mashauri mawili kwa wakati mmoja, bali ulitokana na jitihada za kupata ufafanuzi sahihi wa kisheria kabla ya kuchukua hatua zaidi.
“Kwa kuzingatia yote yaliyoelezwa hapo juu, nimeridhika kuwa waombaji wamewasilisha sababu za msingi, zenye uzito na zinazostahili kuruhusu kuongezewa muda, hivyo maombi ya kuongezewa muda yanakubaliwa,” alisema.
Jaji alisema waombaji ambao ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na AG, wanaelekezwa kuwasilisha maombi yao ya mapitio ndani ya siku tatu kuanzia tarehe ya uamuzi huo, ambayo ni Machi 27, 2026.
