Tahadhari ya usafi wa vyakula minadani yasisitizwa

Maswa. Baadhi ya wananchi wilayani Maswa, mkoani Simiyu, wameiomba Idara ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kuimarisha ukaguzi wa huduma za vyakula vinavyouzwa na mama lishe katika minada mbalimbali, wakidai mazingira ya uandaaji na uuzaji wa chakula si salama kwa afya ya walaji.

Wakizungumza leo, Machi 29, 2026 katika mnada wa Maswa mjini, wananchi hao wamesema katika baadhi ya maeneo chakula huwekwa wazi bila kufunikwa, hali inayokifanya kipigwe na vumbi huku kikiwa karibu na maeneo yenye shughuli nyingi za biashara na mifugo.

Wamesema hali hiyo inaweza kuhatarisha afya za walaji iwapo hatua za kudhibiti usafi wa chakula hazitachukuliwa mapema.

Mkazi wa Kijiji cha Isanga, Paulo Magesa, amesema katika minada mingi chakula huuzwa katika mazingira yasiyozingatia usafi.

Sehemu ya mazingira ya vyakula vinavyopikwa katika mnada wa mjini Maswa. Picha na Samwel Mwanga

“Unakuta wali, maharage au nyama imewekwa wazi kabisa. Watu wanapita, vumbi linapigwa na upepo, lakini chakula kinaendelea kuuzwa. Hii inaweza kusababisha magonjwa,” amesema.

Kwa upande wake, Lenata Maiko amesema licha ya umuhimu wa huduma za mama lishe kwa wafanyabiashara wa minadani, bado kuna haja ya kuboresha mazingira ya uuzaji wa chakula.

“Mama lishe wanasaidia sana, lakini chakula kinapaswa kufunikwa na mazingira yawe safi ili kulinda afya za walaji,” amesema.

Naye George Nyamhanga, mfanyabiashara wa nguo, amesema tatizo jingine ni matumizi ya mifuko ya plastiki kuhifadhi chakula cha moto.

“Wengine huweka chakula kwenye plastiki ili kisipoteze joto, lakini inaweza kuwa na madhara kiafya,” amesema.

Mtaalamu wa afya ya mazingira, Eliza Simba, amesema chakula kinapowekwa wazi kinaweza kuchafuliwa na vijidudu vinavyosababisha magonjwa.

Mmoja wa mamalishe akiendelea na shughuli zake katika mnada wa Maswa mjini. Picha na Samwel Mwanga

“Chakula kinapaswa kufunikwa muda wote ili kuzuia vumbi, wadudu na uchafu mwingine, vinginevyo kinaweza kusababisha magonjwa ya tumbo,” amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa lishe na afya ya jamii, Isack Mrema, ameonya matumizi ya plastiki kwa chakula cha moto, akisema baadhi ya plastiki zinaweza kutoa kemikali hatarishi zinapokutana na joto.

Amesisitiza kuwa pamoja na umuhimu wa biashara za mama lishe, ni lazima usalama wa chakula uzingatiwe, huku akiitaka Idara ya Afya kuongeza ukaguzi na kutoa elimu kwa wauzaji ili kulinda afya za walaji.