Serikali, wadau watuliza hofu ya uhaba wa mafuta

Dar es Salaam. Wakati hofu ya uhaba wa mafuta ikiendelea miongoni mwa wananchi na wafanyabiashara, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo imesema hali ya upatikanaji wa bidhaa hiyo ni ya kuridhisha na hakuna upungufu.

Hofu hiyo imechangiwa na mvutano wa kisiasa Mashariki ya Kati unaohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran, hali iliyozua wasiwasi wa kupanda kwa bei na upatikanaji wa mafuta katika baadhi ya nchi za Afrika.

Akizungumza leo Machi 29, 2026 wakati wa ziara katika vituo vya kuhifadhi mafuta Kigamboni, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amesema taarifa za ucheleweshaji wa huduma katika baadhi ya vituo hazimaanishi kuwepo kwa uhaba.

“Hakuna mabadiliko ya msingi katika utoaji wa huduma. Mafuta yanatolewa kulingana na mwenendo wa mahitaji ya kawaida,” amesema Mwenda.

Ameeleza kuwa changamoto inayoonekana kwa sasa inatokana na ongezeko la mahitaji kutoka kwa wafanyabiashara, huku TRA ikijipanga kuongeza ufanisi kwa kufanya kazi saa 24 inapobidi ili kuhudumia soko la ndani na nchi jirani.

Kwa upande wake, Meneja wa Uhifadhi na Usambazaji wa Camel Oil Tanzania Limited, Anwar Abeid, amesema kampuni hiyo inaendelea kutoa huduma kama kawaida na haina upungufu wa mafuta.

Amefafanua kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiongeza ghafla mahitaji yao, jambo linalosababisha changamoto ya kuwahudumia kwa wakati mmoja.

“Tunatoa mafuta kulingana na mahitaji ya awali. Mteja aliyekuwa akinunua kiasi kidogo akihitaji mara mbili ghafla, ni lazima kuwe na uwiano ili wengine pia wapate huduma,” amesema.

Naye Meneja wa Nchi wa Moil Energies, Sajed Habib Rai, amesema hali ya mafuta nchini ni tulivu, akibainisha kuwa kuna meli tatu zenye shehena ya mafuta zikiwa nje ya bandari zikisubiri kushusha mizigo.

Amesema petroli ipo ya kutosha, huku changamoto ndogo ikionekana upande wa dizeli kutokana na ongezeko la mahitaji, lakini hatua zimechukuliwa kuongeza upatikanaji wake.

“Ndani ya wiki ijayo kutakuwa na uhakika wa mafuta ya kutosha katika vituo vyote,” amesema.

Akijibu tuhuma za wafanyabiashara kuficha mafuta wakisubiri kupanda kwa bei, Rai amesema madai hayo si ya kweli, akisisitiza kuwa mafuta yote yaliyopo yanasimamiwa na mamlaka husika na kiwango chake kinajulikana.

Wakati huohuo, Kamishna wa Forodha wa TRA, Juma Hassan, amesema mamlaka hiyo imeanzisha mfumo mpya wa kusimamia mafuta unaolenga kuongeza uwazi na kudhibiti mapato ya Serikali.

Amesema mfumo huo unahakikisha mafuta yote yanayoingia sokoni yanalipiwa kodi kabla ya kuuzwa, huku yale ya kusafirishwa yakifuatiliwa ili yasibaki nchini kinyume cha sheria.

“Hatua hii inalenga kuhakikisha kila lita ya mafuta inazingatia taratibu zote za kisheria,” amesema.

Ameongeza kuwa vituo vya kuhifadhi mafuta vinatakiwa kuwasilisha mipango ya upakiaji na taarifa za mauzo ya kila siku, hatua inayowezesha TRA kufuatilia mwenendo wa bidhaa hiyo kwa karibu.

Hassan amesisitiza kuwa mfumo huo haucheleweshi usambazaji, bali unaimarisha nidhamu, uwazi na ufanisi katika sekta ya mafuta.