Dar es Salaam. Serikali imeahidi kuendeleza dhamira yake ya kulinda, kuimarisha na kuboresha masilahi ya wataalamu wa afya nchini, ikilenga kuongeza motisha, ufanisi na ubora wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Machi 28, 2026, wakati wa hafla ya chakula cha jioni na madaktari bingwa pamoja na wataalamu wa afya, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imejipanga kuimarisha mazingira ya kazi kwa wataalamu wa afya ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi.
Amesema mafanikio ya sekta ya afya yanategemea kwa kiasi kikubwa ustawi wa watumishi wake, hivyo juhudi zinaelekezwa katika kuboresha masilahi yao ikiwa ni pamoja na mazingira ya kazi, mafunzo na upatikanaji wa vitendea kazi vya kisasa.
“Tunatambua mchango mkubwa wa watumishi wa afya katika kuokoa maisha ya Watanzania, hivyo Serikali itaendelea kuwawezesha ili kuongeza tija na ubora wa huduma,” amesema Mchengerwa.
Kwa kuzingatia mjadala mpana unaoendelea miongoni mwa wadau wa afya, zipo changamoto kadhaa zinazowakumba watumishi wa sekta hiyo ambazo zinahitaji kushughulikiwa kwa haraka ili kuboresha utendaji wao na huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Delilah Kimambo , wakati wa hafla ya chakula cha jioni na madaktari bingwa pamoja na wataalamu wa afya, iliyofanyika Johari Rotana.
Baadhi ya wataalamu wa afya waliozungumza na Mwananchi (hawakutaka kutaja majina), wametaja suala la posho na stahiki mbalimbali kuwa bado ni changamoto.
Pia wamezungumzia mazingira ya kazi kutoridhisha ipasavyo, wakitaja upungufu wa vifaa tiba, msongamano wa wagonjwa na uhaba wa watumishi husababisha mzigo mkubwa wa kazi, hali inayochangia uchovu na wakati mwingine makosa ya kitaalamu.
“Kuna shida ya posho ya nyumba kwa baadhi ya watumishi haikidhi gharama halisi za maisha, hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, hali inayotulazimu kuishi mbali na maeneo ya kazi au katika mazingira yasiyo rafiki,” amesema muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana.
Pia baadhi yao wametaja upatikanaji wa mikopo nafuu kupitia taasisi za Serikali kama Hazina bado ni mgumu au hauwafikii watumishi wote wanaostahili, jambo linalopunguza uwezo wao wa kuboresha maisha na ustawi wao binafsi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali inaendelea kuimarisha mpango wa mafunzo ya madaktari bingwa na bobezi kupitia Mpango wa Samia Health Super-specialization, unaolenga kuongeza wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, katika mwaka wa masomo 2025/2026, jumla ya wataalamu 1,483 wanasomeshwa katika fani mbalimbali za ubingwa na ubobezi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuboresha huduma za afya nchini.
Ameeleza kuwa tangu mwaka wa masomo 2015/2016 hadi 2025/2026, wataalamu 8,989 wamefaidika na ufadhili wa Serikali, huku mafunzo hayo yakitolewa katika hospitali za Taifa, kanda na maalumu ili kuhakikisha huduma zinatolewa na wataalamu waliobobea.
“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa urahisi zaidi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu au kwenda nje ya nchi,” amesema.
Baadhi ya madaktari bingwa pamoja na wataalamu mbalimbali wa afya , wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika Johari Rotana.
Aidha, amesema Serikali imeongeza idadi ya watumishi wa sekta ya afya hadi kufikia 182,430, ambapo asilimia 78 wapo katika ngazi ya afya ya msingi, asilimia 19 hospitali za rufaa na asilimia tatu katika vyuo, wakala na idara za Wizara ya Afya.
Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo yote ya nchi, hususan vijijini ambako mahitaji ya huduma bado ni makubwa.
Mchengerwa pia ametoa wito kwa wataalamu wa afya kuendelea kujituma na kuhakikisha wanalea kizazi kipya cha wataalamu wenye ubora wa juu, akisisitiza kuwa ubingwa wa kweli hupimwa kwa mchango wa kukuza wataalamu wengine.
Sambamba na hilo, amehamasisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya afya katika kuendeleza tafiti, mafunzo na matumizi ya teknolojia za kisasa, ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa nchini.