Profesa Lipumba akabidhi mikoba CUF, asema hana imani na Katibu Mkuu

Dar es Salaam. Hatimaye, Profesa Ibrahim Lipumba amekubali kung’olewa katika wadhifa wa uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), huku akiacha maagizo matano kwa mwenyekiti mpya, Mirambo Yusuf, likiwemo kuhakikisha anasimamia nchi kupata Serikali ya mpito.

Mbali na hilo, ameisisitiza upatikanaji wa Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi, kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, na wanachama kuwa kitu kimoja katika kuijenga taasisi. Pia, amependekeza Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Hamad Masoud, kung’olewe kwa madai ya kukosa sifa ili kurejesha imani ndani ya chama ambacho kimekumbwa na migogoro ya kiuongozi.

Profesa Lipumba, aliyeshika wadhifa huo kwa miaka 27, ametoa kauli hiyo ikiwa siku 42 (mwezi mmoja na siku 12 ) zimepita baada ya kung’olewa madarakani kufuatia maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Uamuzi wa Msajili, uliotolewa Februari 13, 2026, wa kutengua uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika Desemba 18 na 19, mwaka jana uliohusisha pia ushindi wa Profesa Lipumba na wenzake, kwa hoja kuwa hawakupata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wajumbe wa mkutano mkuu.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa chama Cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwamakao makuu ya chama hicho, Buguruni Jijini Dar es Salaam kukabidhi ofisi rasmi kwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Mirambo Yusuf

Kwa mujibu wa maelekezo hayo, ambayo yalisababisha mgawanyiko ndani ya chama kati ya waliounga mkono na waliopinga, mchakato wa uchaguzi huo ulipaswa kurudiwa ili kuzingatia taratibu, kanuni na katiba ya chama, lakini hatua hiyo haikuchukuliwa.

Hivyo, Februari 20 na 21 mwaka huu ulifanyika mkutano rasmi wa kumng’oa Profesa Lipumba, ambao hakuhudhuria. Washirika wake walidai kuwa walikuwa wanakwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili kwa kuwa hawakupewa nafasi ya kujitetea.

Katika kipindi chote hicho, Profesa Lipumba alikaa kimya hadi Mirambo alipochaguliwa na kuanza kazi. Baada ya siku 42, amejitokeza hadharani na kukubali rasmi kuondolewa kwake.

Akizungumza Dar es Salaam Leo Machi 29,2026 na vyombo vya habari katika makao makuu ya chama wakati wa kukabidhi ofisi kwa mwenyekiti mpya, Profesa Lipumba amesema kuwa licha ya mchakato wa kuondolewa kwake kuwa na dosari, hana wasiwasi na uongozi mpya.

“Ingawa mchakato wa kuning’oa ulikuwa wa kimagumashi, Binafsi kikatiba na utendaji sina wasiwasi na mwenyekiti mpya na viongozi waliochaguliwa wala sijasema kama sijatendewa haki, ila naweza kusema amnyimaye punda mbaazi basi unaweza kumalizia mwenyewe,” amesema Profesa Lipumba

Amesema, taratibu za kuitisha mkutano mkuu hazikuwa nzuri hata mwaka 2024 hakutamani kugombea tena nafasi hiyo, hivyo kitendo cha kumwondoa wamepunguza mzigo wake.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa mchakato huo ulikuwa na dosari kwa kuwa hauwezi kuhalalisha uchaguzi wa Desemba 2024 halafu ukautengua wa Februari 2026.

Amesema chanzo cha kuondolewa kwake ni hotuba aliyotoa Januari 27, 2026, ambapo chama kilipendekeza kuwepo kwa serikali ya mpito itakayoiwezesha nchi kufanya uchaguzi mwingine.

“Hotuba ile iliwakera baadhi ya watu wenye ushawishi, ndipo wakaandaa mkakati wa kuniondoa haraka bila kufuata utaratibu,” amesema.

Kuhusu maagizo yake, Profesa Lipumba ametoa wito kwa uongozi mpya kuhakikisha kunapatikana katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi, pamoja na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Pia amesisitiza kujadili msimamo wa chama kuhusu kuundwa kwa serikali ya mpito, akidai kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 haukuwa huru na wa haki.

Amemtaka mwenyekiti mpya kuchunguza uhalali wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Hamad Masoud, akidai kuwa alishindwa kutekeleza majukumu muhimu alipoteuliwa kugombea urais Zanzibar.

“Alitukosesha kuwa na mgombea urais Zanzibar mwaka uliopita hatuwezi kuwatangazia wananchi huyu ndiye atakayetuvusha tutajimaliza, hilo naomba na nimelisema hadharani kusudi niweze kueleweka wazi lakini ndiyo ukweli huwezi kuteuliwa kuwa mgombea urais ukashindwa kurudisha fomu, hivyo tukimuacha kwenye nafasi hiyo tumekwisha,” amesema.

Hata hivyo, Masoud amejibu hoja ya Profesa Lipumba akisema hizo ni hasira zake kwake kwa kuwa anamjua nje ndani na anahofia akishika wadhifa huo anaweza kufichua maovu yake mengi.

“Profesa Lipumba namjua nje ndani na siri zake nyingi hivyo ana hofu kubwa baada ya mimi kuteuliwa kushika nafasi hii, anaona nitafichua, najua mengi kwanza chama nilikikuta kiko chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi,” amemjibu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mirambo Yusuf amempongeza Profesa Lipumba kwa mchango wake mkubwa ndani ya chama kwa kipindi chote cha miaka 27.

Amesema chama kinatambua mchango wake na kitaendelea kumpa nafasi ya kutoa ushauri na mawazo yake.

Mirambo ameongeza kuwa wamepokea ushauri wote uliotolewa na utawasilishwa kwenye vikao halali vya chama kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi.

“Tutayajadili kwa mujibu wa taratibu za chama, na maamuzi yatategemea wakati na mwelekeo wa wanachama,” amesema.

Pia Mirambo amewataka wanachama kuacha migogoro na kuungana kwa ajili ya kufanikisha malengo ya chama ya kushika dola.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa chama Cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa makao makuu ya chama hicho, Buguruni Jijini Dar es Salaam kukabidhi ofisi rasmi kwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Mirambo Yusuf

Kwa upande mwingine, Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi, Daud Hassani, amesema uteuzi wa Katibu Mkuu ulifanyika kwa kufuata taratibu za chama, ambapo mwenyekiti alipendekeza majina na Baraza Kuu likaidhinisha kwa kura.

Amesema Mwenyekiti na timu yake wamemuamini Masoud na walishauriana na walileta jina lake Baraza Kuu na wakamchagua, hoja ya Profesa Lipumba haina nguvu na alichozungumza ni maoni kama mwanachama mwingine wa kawaida.

Hassan amesema madai ya Profesa kuwa hana imani naye kulikana na makosa aliyotenda Baraza Kuu halina ushahidi wa hizo tuhuma huku akimtaka atulie kwani kila zama na kitabu chake, Mirambo amemchagua Masoud kwa kuwa anaweza kufanya naye kazi.

“Profesa Lipumba ni mwanachama wa kawaida, anachokizungumza anashindwa kuheshimu mamlaka ya Baraza Kuu lililomchagua Masoud anataka kupokea nguvu zake hatutakubali, baraza ni chombo kikubwa ambacho lazima kiheshimiwe kikifanya uamuzi,” amesema.