Mastaa Dar City watoa onyo BAL 2026

MABINGWA wa kikapu wa Tanzania, Dar City wanatarajiwa kushuka tena dimbani kesho watakapokutana na Al Ahly Ly ya Libya katika mwendelezo wa mashindano ya BAL 2026 nchini Afrika Kusini.

Mchezo huu utapigwa wakati Dar City wakiwa kwenye kiwango bora baada ya kuanza msimu kwa ushindi wa michezo miwili mfululizo, hali inayowaweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania kufuzu hatua ya mtoano. Katika michezo miwili iliyopita, Dar City iliifunga Johannesburg Giants pointi 100–70 kabla ya ushindi dhidi ya Nairobi City Thunder kwa pointi 90–85.

Ushindi huo wa pili ulionyesha uimara wa Dar City, hasa waliporudi kutoka nyuma na kuibuka na ushindi katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Kwa upande mwingine, Al Ahly Ly wataingia katika mchezo huo wakiwa kwenye presha baada ya kupoteza michezo miwili ya mwanzo.

Timu hiyo ya Libya ilipoteza kwa RSSB Tigers (103-95) kabla ya kuchapwa tena na Petro de Luanda (104-90) huku changamoto kubwa ikiwa ni safu yao ya ulinzi kuruhusu zaidi ya pointi 100 katika kila mchezo.

Nahodha wa Al Ahly Ly, Sofian Hamad amekiri kuwa wanahitaji kuboresha haraka eneo hilo kama wanataka kurejea kwenye ushindani.

Dar City wataingia wakiwa na morali ya juu huku wakitegemea kasi yao na ubora wa wachezaji kama David Michineau (Point Guard) ndiye injini ya timu ‘playmaker mkuu’, ana uwezo wa kufunga na kuandaa mashambulizi, alifunga pointi 39 dhidi ya Nairobi City Thunder.

Nyota mwingine ni Michael Foster Jr. (Forward), ni mchezaji mwenye nguvu na uzoefu wa NBA, Nisre Zouzoua (Shooting Guard) ana uwezo mkubwa wa mitupio ya mbali (3-pointers) na Daniel Utomi (Forward) ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa la Nigeria na Hasheem Thabeet (Center) ambaye katika mchezo dhidi ya Nairobi City Thunder aliokoa mchomo mmoja wa hatari.

Nyota wa Dar City, Michael Foster ambaye alifunga pointi 10 na ‘rebounds’ 8, amesema; “Tunataka kuweka historia na kuwa bora zaidi, tuna uwezo wa kushinda mechi zote.”

Amin Mkosa amesema: “Kila mmoja wetu katika kikosi anajua jukumu lake ni lipi na kwa nini tupo hapa, tumekuwa tukijipanga katika kila mchezo kwa umakini na kujitahidi kushinda kwa pamoja. Uwezo wetu ni mkubwa na tunataka kuendelea kushinda ili kufikia malengo yetu.”