Waziri Kairuki awang’ata sikio waandishi wa habari wanawake

Dar es Salaam. Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amewataka wanawake wanahabari nchini kuhakikisha kuwa ‘Kongamano la Malkia wa Habari’ halibaki kuwa tukio la siku moja, bali linakuwa chachu ya mabadiliko ya kudumu katika taaluma na maisha yao.

Kongamano hilo lilikuwa fursa kwa waandishi wa habari kushiriki uzoefu wao kupitia midahalo na majadiliano yaliyofanyika katika hafla hiyo.

Akizungumza Machi 28, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano hilo, Kairuki amesema ni muhimu kujenga mfumo endelevu wa kusaidiana, ikiwemo kuanzisha programu za usimamizi wa kuwezesha wanahabari chipukizi kukua kitaaluma na kiuchumi.

Amesema hiyo itaongeza mshikamano na kuinua kiwango cha taaluma ya uandishi wa habari kwa wanawake, huku akihimiza pia kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa kifedha utakaowasaidia wanahabari wakati wa shida na kuwawezesha kuwekeza katika miradi ya maendeleo.

Mratibu wa Kongamano la Malkia wa Habari, Penina Malundo (kushoto) akizungumza na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia  ya Habari, Angellah Kairuki (Katikati) pamoja na Mhariri wa habari za Siasa gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka. 

“Tusibaki kwenye gala au kukutana tu, bali tujenge mifumo ya kusaidiana katika shida na raha ili wale wanaochipukia wapate nafasi ya kukua na waliokomaa waweze kutumia uzoefu wao kuwainua wengine,” amesema Kairuki.

Pia, Waziri huyo amesema mafanikio katika sekta ya habari hayawezi kupatikana kwa mtu mmojammoja, bali kwa nguvu ya pamoja na kuwahimiza wanahabari wanawake kuunda mitandao ya kitaaluma inayolenga maeneo maalumu kama vile Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,  uchumi wa kidijitali na akili unde (AI).

Kairuki amewataka washiriki wa kongamano hilo kujitafakari kuhusu mchango wao katika jamii, hususan katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wanawake, wasichana na vijana.

Amesema wanahabari wana nafasi ya kipekee ya kuibua masuala ambayo hayapewi kipaumbele na kuyapa sauti, hivyo kuchangia katika utatuzi wa changamoto za kijamii.

“Kupitia taaluma hii, kila mmoja ajiulize amefanya nini kuleta athari chanya katika maisha ya wanawake na jamii kwa ujumla,” amesema.

Katika hatua nyingine, amehimiza wanahabari wanawake kutumia vyema fursa ya uwepo wa uongozi wa juu wa wanawake nchini kusukuma ajenda zao za maendeleo.

Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana nao kupitia wizara na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa na sekta ya habari inakuwa chachu ya maendeleo ya Taifa.

Waandishi wa habari wanawake wakiwa wakiwa wanacheza kwenye Kongamano la Malkia wa Habari lililofanyika jana Machi 28, 2026 jijini Dar es Salaam

Kuhusu mustakabali wa kongamano hilo, Kairuki amesema huo ni mwanzo wa safari, amehimiza waandaaji kuhakikisha unakuwa wa kila mwaka na wenye matokeo yanayoonekana.

Amewataka washiriki kuondoka na mpango kazi utakaotekelezeka, badala ya kubaki na kumbukumbu za tukio pekee kwani hilo si tukio la mara moja, bali ni mwanzo wa mchakato unaopaswa kuendelezwa kila mwaka kwa vitendo na matokeo.

Kwa upande wake mratibu wa kongamano hilo, Penina Malundo amesema lengo ni kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili waandishi wa habari wanawake kushirikiana katika shughuli za kijamii na kusaidia kuinua sauti ya wanawake katika vyombo vya habari.

Naye, Mhariri wa habari za siasa  wa gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka akizungumza katika mdahalo amewataka waandishi wa habari wanawake kutokubali kukatishwa tamaa kwa upande wa habari za uchunguzi.

“Uandishi ni kuamini kwenye jambo unalofanya usikubali baadhi ya watu kukukatisha tamaa ukiona umetoa wazo la habari na wakasema apewe mwanaume waambie nitafanya na huyo mwanaume atakuja baadaye,” amesema Timbuka.

Mwandishi wa habari za biashara na takwimu wa gazeti la Mwananchi, Aurea Simtowe amesema uandishi wa sasa unahitaji kusoma hususan matumizi ya akili unde (AI) ambayo inakuwa kwa kasi.

“Tunahitaji kujifunza vitu vipya kila siku ili kufanya kazi kwa haraka na wepesi hivyo muhimu kutumia AI ambayo inafanya habari ngumu kuwa laini kwa wasomaji wetu bila kusahau kutumia ubinadamu kuleta uhalisia wa taarifa tunazofanya,” amesema Aurea.

Mhariri Mkuu wa Clouds Media, Joyce Shebe amewaasa wanawake kutafuta mbinu mbalimbali za kupambana na taarifa hasi za mitandaoni ambazo kwa sasa zinaongezeka kila siku.