Ngorongoro waanzisha mfuko wa elimu kusaidia wanafunzi wasiojiweza

Arusha. Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha imeanza hatua za kuanzisha mfuko maalumu wa elimu utakaolenga kuwasaidia watoto wa jamii ya Kimasai kutoka familia zenye kipato cha chini kuendelea na masomo ya sekondari.

Mpango huo endelevu umeanzishwa na Mbunge wa Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, unatarajiwa kuwanufaisha wanafunzi 280 katika awamu ya kwanza, watakaochaguliwa kutoka kata mbalimbali kwa kuzingatia ufaulu wa kitaaluma pamoja na uhitaji wa kifedha.

Akizungumza katika kikao maalumu kilichowakutanisha wadau wa maendeleo ya elimu mkoani Arusha leo Machi 29, 2026, Ndoinyo amesema mfuko huo utasaidia wanafunzi waliofaulu vizuri elimu ya msingi, lakini wanashindwa kuendelea na sekondari kutokana na changamoto za kifedha.

Amesema mfuko huo utagharamia mahitaji muhimu ya wanafunzi, yakiwemo sare za shule, vifaa vya kujifunzia na mahitaji mengine ya msingi, ili kuwawezesha kuanza safari ya elimu ya sekondari kwa utulivu na kujiamini.

“Tuko hapa kuweka mikakati madhubuti ya uanzishwaji, uendeshaji na uendelevu wa mfuko huu, ili kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga na sekondari wanapata mahitaji yote muhimu ya msingi,” alisema Ndoinyo.

Amebainisha kuwa wazo la kuanzisha mfuko huo lilitokana na maombi mengi aliyoyapokea mwaka 2025 kutoka kwa wazazi waliokuwa wakishindwa kuwapeleka watoto wao shule licha ya kufaulu vizuri.

Ndoinyo amesema kabla ya mpango huo, aliendesha juhudi binafsi zilizowezesha kusaidia wanafunzi 80, wakiwemo wavulana 40 na wasichana 40, lakini mahitaji yameendelea kuongezeka.

“Ndiyo maana nimeona umuhimu wa kuwakutanisha wadau ili tuanzishe mfuko wa kudumu utakaosaidia wanafunzi wengi zaidi wenye ufaulu mzuri lakini wasio na uwezo wa kujigharamia,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya juhudi za Serikali kuondoa ada na baadhi ya michango shuleni, bado baadhi ya familia, hasa katika jamii za wafugaji, zinashindwa kumudu gharama za mahitaji binafsi ya wanafunzi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Mohamed Hussein, amepongeza hatua hiyo akisema inaunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika elimu kwa kuajiri walimu zaidi ya 20,000, kujenga zaidi ya madarasa 30,000 pamoja na mabweni, hususan kwa wanafunzi kutoka jamii za wafugaji.

“Hatua hii ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika kuimarisha upatikanaji wa elimu bora kwa makundi yote ya jamii,” amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Manja Yaile, amesema watahakikisha mfuko huo unasimamiwa kwa uwazi na ufanisi ili rasilimali zitakazochangwa ziwanufaishe walengwa.

“Tutahakikisha mfuko unakuwa wa kuaminika na wenye matokeo chanya yatakayodhihirika kupitia mafanikio ya wanafunzi watakaonufaika,” alisema.