CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA KAMPASI YA SINGIDA CHATOA MSAADA KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM.

Machi 28, 2026 Na Mwandishi Wetu, Singida

Kampasi ya Singida ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) imekabidhi msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum wanaolelewa katika Kituo cha Malaika wa Matumaini kilichopo Ititi, mkoani Singida, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.

Zoezi hilo limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, akishirikiana na Mkurugenzi wa Kampasi ya Singida, Dkt. Emmanuel Tandika, pamoja na watumishi wa chuo hicho. Msaada huo umewajumuisha vyakula mbalimbali kama mchele, sukari, unga wa sembe na vifaa vya usafi, na umetolewa sambamba na zoezi la kufanya usafi katika mazingira ya kituo hicho.

Mhe. Gondwe, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, ametoa pongezi kwa Kampasi ya Singida kwa kuonyesha moyo wa kujitolea na kuguswa na jamii, akisema kitendo hicho kimekuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine katika mkoa huo.

“Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, tunapongeza kazi iliyofanywa na Chuo cha Utumishi wa Umma. Utoaji huu wa msaada umeonyesha upendo wa kweli kwa watoto hawa na umeunga mkono juhudi za serikali katika kuwajali makundi maalum,” amesema Mhe. Gondwe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampasi ya Singida, Dkt. Emmanuel Tandika, amesema msaada huo umetolewa kama sehemu ya mchango wa chuo kwa jamii inayolizunguka.

“Tunaposherehekea miaka 25 ya kutoa huduma kwa umma, tumeona ni vyema kuonyesha upendo na mshikamano kwa watoto hawa wenye mahitaji maalum wajue kuwa hawako peke yao, jamii ipo pamoja nao na inawapenda.” Amesema Dkt. Tandika

Aidha, ameeleza kuwa msaada huo umetolewa pia ili kuwapa motisha masista na walezi wanaohudumia watoto hao licha ya changamoto wanazopitia kila siku.

Mlezi wa kituo hicho, Sista Rosalia Nicodemus, kwa niaba ya Mkuu wa Shirika, ameshukuru uongozi wa chuo na serikali ya mkoa kwa msaada huo, akisema umeleta faraja na matumaini kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo.

“Kupokelewa kwa wageni kama hawa kumewatia moyo sana watoto wetu,” amesema. “Kwa kweli wamejisikia kupendwa na kuthaminiwa, jambo ambalo limewasaidia kupata nguvu mpya ya kuendelea.”

Sista Rosalia pia ametoa shukrani kwa wadau mbalimbali waliotoa misaada mingine, akiwahamasisha taasisi na watu binafsi kuendelea kushirikiana na kituo hicho kwa kutoa misaada na upendo.

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kimeendelea kufanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kampasi zake za Dar es Salaam, Tabora, Tanga, Singida, Mtwara na Mbeya, kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 25 kitakaofanyika mwezi Juni 2026.