Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali haina mpango wa kuliuza eneo la Coco Beach kwa mwekezaji yeyote, bali inalenga kuliboresha kwa manufaa ya wananchi.
Kauli ya Mwigulu inakuja baada ya hofu iliyoibuka kutoka kwa wafanyabiashara wa fukwe hiyo, wakisema Manispaa ya Kinondoni iliwapa notisi ya siku 30 waondoke katika eneo hilo bila maelezo ya kina, hivyo waliamini imeuzwa kwa mwekezaji.
Katika taarifa hiyo, wamesema uongozi wa manispaa hiyo umechukua namba za simu za baadhi yao, kuwaeleza utawapa kiasi cha fedha na hawatatakiwa kurudi tena fukweni hapo, waondoke kwenda maeneo mengine.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akitoa ufafanuzi rasmi kuhusu hatma ya eneo la Coco Beach, akisisitiza kuwa halitauzwa kwa mwekezaji yeyote bali maboresho yatafanyika kwa manufaa ya wananchi waliopo katika eneo hilo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, aliwahi kukanusha hilo, akisema manispaa haina mpango wa kuuza eneo hilo, bali inaliboresha baada ya kuanza kumomonyoka kutokana na shughuli zinazoendelea.
Katika ufafanuzi wake huo, amewahakikishia wafanyabiashara kuwa hakuna mpango wa kuuza eneo hilo, kitu pekee kitakachoruhusiwa ni uendeshaji kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
“Tunachotamani patengenezwe vizuri, biashara zifanyike mchana na usiku, pawepo na huduma ya mawasiliano ya intaneti. Niwaombe tuondoe hofu na tusikubali kupotoshwa,” amesema.
Mwigulu ameeleza hayo leo, Machi 29, 2026, alipotembelea eneo hilo jijini Dar es Salaam na kuzungumza na wajasiriamali wadogo wanaofanya shughuli zao katika fukwe hiyo.
“Coco Beach haiuzwi. La kwanza, niwaondolee hofu, hapauzwi wala hakuna mwekezaji mwingine zaidi yenu ninyi wenyewe. Hakuna atakayekuja kutoa maelekezo zaidi ya yale yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan. Hapa hapauzwi,” amesisitiza.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akitoa ufafanuzi rasmi kuhusu hatma ya eneo la Coco Beach, akisisitiza kuwa halitauzwa kwa mwekezaji yeyote bali maboresho yatafanyika kwa manufaa ya wananchi waliopo katika eneo hilo.
Ameeleza Serikali itaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wananufaika na maboresho yanayofanyika katika eneo hilo.
“Sisi wasaidizi wa Rais tutaendelea kuhakikisha Watanzania wanapata lile tabasamu la mama ambalo amewaahidi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amewataka watendaji wa Manispaa ya Kinondoni kubadili mtindo wa utendaji kazi kwa kuwafuata wananchi moja kwa moja badala ya kuwasubiri ofisini.
“Ninatoa agizo kwa mkuu wa wilaya, mkurugenzi, ofisa biashara na watendaji wengine: msikae ofisini tu. Tokeni mkazungumze na wananchi hawa moja kwa moja pale wanapokuwa na masuala yanayowahusu,” amesisitiza.
Amewahimiza wajasiriamali wa eneo hilo kuunga mkono juhudi za Serikali katika maboresho yanayoendelea kufanyika, huku akisisitiza kuwa fursa zitakazotokana na maboresho hayo zitawanufaisha wao wenyewe.