Dar es Salaam. Wachambuzi wameeleza kuwa kitendo cha Tanzania kushikilia daraja lake la mikopo la B+ lenye mtazamo thabiti ni ishara ya uchumi unaokua kwa kasi ya wastani, huku ukiwa na viwango vinavyodhibitiwa vya deni la Taifa.
Shirika la tathmini ya mikopo la Fitch Ratings, Machi 27, 2026, lilithibitisha daraja la muda mrefu la mikopo ya fedha za kigeni (LTFC) kwa Tanzania kuwa “B+” likiwa na mtazamo thabiti, lakini wachumi wanasema bado kuna changamoto za kimuundo zinazozuia kasi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, daraja hilo ni ishara ya uwiano kati ya juhudi za mageuzi zinazoendelea na udhaifu unaoendelea kujitokeza, hali inayoashiria kuwa nafasi ya mikopo ya nchi haitabadilika kwa kiasi kikubwa kwa muda mfupi isipokuwa mabadiliko ya kina yafanyike.
Wataalamu wa uchumi wanaona matokeo hayo kama ishara ya uthabiti badala ya kudumaa kwa uchumi, wakieleza kuwa kuna mwendelezo wa ukuaji pamoja na umuhimu wa kuimarisha zaidi sera za kifedha na taasisi.
Mhadhiri mwandamizi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Tobias Swai, anasema mtazamo huo thabiti unatoa matumaini ya tahadhari, ukionesha kuwa nchi ipo katika mwelekeo unaoweza kusababisha kupandishwa daraja endapo mageuzi yataendelezwa.
Anataja utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama vichocheo muhimu vya kuimarisha msingi wa uchumi.
“Hatua za hivi karibuni za ksera, ikiwamo kuhimiza matumizi ya shilingi ya Tanzania katika miamala ya ndani na kutekeleza mageuzi ya kodi, zinasaidia kuleta utulivu wa uchumi na kuboresha mwenendo wa mapato ya serikali,” anasema, akiongeza kuwa maendeleo endelevu yanaweza kuathiri vyema tathmini za baadaye.
Daraja hilo pia linaakisi ukuaji mzuri wa Pato la Taifa (GDP) na mfumuko mdogo wa bei, hali inayochangiwa na mageuzi pamoja na upatikanaji wa fedha kutoka nje kupitia mpango wa International Monetary Fund (IMF). Hata hivyo, linazuiwa na changamoto za utawala, mapato madogo ya serikali na udhaifu wa sera za uchumi mpana unaosababisha misukosuko katika soko la fedha za kigeni.
Mchambuzi huru wa masuala ya fedha, Christopher Makombe, anasema tathmini hiyo inaonesha uchumi unaofanya vizuri kwa kiasi, lakini bado una vikwazo vya kimuundo.
“Ushirikiano huu unawapa wawekezaji uhakika kwamba mageuzi yataendelea kuwa kwenye mstari sahihi,” anasema.
Hata hivyo, anaonya kuwa changamoto kama ukusanyaji mdogo wa mapato ya ndani, masuala ya utawala na akiba ndogo ya fedha za kigeni bado zinaathiri taswira ya mikopo ya nchi.
Kwa mujibu wa makadirio ya Fitch, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia sita mwaka 2026 na 2027, ukichochewa na sekta za kilimo, madini na uwekezaji katika miundombinu mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR) na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.
