KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge ametua nchini na kuanza na rekodi ya aina yake akiwa hajapoteza mechi ndani ya dakika 90 dhidi ya timu zilizomaliza ndani ya tano bora msimu uliopita, huku akisema kazi waliyo nayo ni kuendelea kuonyesha utofauti.
Azam haijafungwa na Yanga kwenye mzunguko wa kwanza ikipata suluhu, imepata pointi tatu mbele ya Simba ugenini kwenye mzunguko wa kwanza, imepata sare nyumbani dhidi ya Singida Black Stars, ikaichapa TRA United nyumbani.
Azam ni moja ya timu chache za Ligi Kuu Bara ambazo zilianza msimu na kumaliza raundi ya kwanza na kocha mmoja ambaye ni Ibenge, huku rekodi zikimpa nafasi ya kutumikia mkataba wa mwaka mmoja aliosaini na klabu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge amesema kikosi hicho katika msimu huu kina mabadiliko makubwa siyo tu ya uchezaji. bali hata mchezaji mmoja mmoja.
Amesema akiwa kocha furaha yake ni kuona timu kubwa zinavunjwa nguvu zilizonazo na timu anayoifundisha, hivyo sio jambo lililotokea tu mpaka kufikia rekodi waliyokuwa nayo, bali imetokana na mipango mathubuti katika viwanja vya mazoezi.
“Bado tunakazi kwenye mechi za marudiano dhidi ya timu hizo na malengo yetu makubwa ni kuendelea kuonyesha tofauti dhidi ya timu za juu na naamini wachezaji wetu wataendelea kuimarika kuonyesha ubora uwanjani,” amesema.
“Malengo yetu ni kuwa katika nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi, lakini ya chini ni kupunguza tofauti ya pointi kati yetu na Simba na Yanga walio juu yetu.
“Kwa sasa hatutakiwi kuwa na utofauti mkubwa wa pointi, labda ziwe nne tofauti na msimu uliopita zilikuwa 15, ni nyingi sana. Azam haitakiwi kuwa na hali kama hiyo. Tunatakiwa kufanya kazi sana kutimiza malengo yetu haya.”
Azam FC inapamba kufikia malengo na kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa imecheza mechi 15 ikifikisha pointi 29. Timu hiyo imeshinda mechi saba, sare nane na haijapoteza ikiwa chini ya Simba (31) na Yanga (38).
