Keshokutwa Jumatano Aprili Mosi 2026, Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuendelea ambapo kwa mwezi huo pekee hadi unakamilika, kuna kitu kinaweza kuamuliwa kwa baadhi ya timu zinazoshiriki ligi hiyo.
Hadi ligi inasimama kupisha mechi za Kalenda ya FIFA, Yanga ilikuwa kileleni mwa msimamo ikikusanya pointi 38, wakati KMC ikiburuza mkia na pointi nane, timu hizo mbili na nyinginezo zimeshacheza mechi zote 15 za duru la kwanza, ni Simba pekee ina mechi pungufu ya moja ikishuka dimbani mara 14.
Lakini pia, JKT Tanzania, Mtibwa Sugar, Namungo, Dodoma Jiji, Mashujaa na Tanzania Prisons, zimecheza zaidi ambapo kila moja ina mechi 17.
Kwa kifupi, timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu, asilimia kubwa hivi sasa zimeanza hesabu za duru la pili ikiwa ni kipindi cha kuweka mambo sawa kuelekea mwisho wa msimu.
Wakati hesabu zikianza kuwekwa sawa, mwezi Aprili kwa kiasi kikubwa umeshikilia hatma ya kuukimbilia ubingwa, lakini pia kujiepusha na janga la kushuka daraja kwa zile timu nne ambazo mbili za nafasi ya 15 na 16 zinazoshuka moja kwa moja, huku zile za 13 na 14 zikilazimika kucheza mtoani kuwania kubaki.
Kule juu kwenye msimamo ukiiweka kando Yanga, Simba inafuatia na pointi 31, kisha Azam yenye 29, huku Singida Black Stars iliyopo nafasi ya sita ikitokea imeshinda mechi moja ili kuwa sawa na Mtibwa Sugar kimichezo, basi itapanda hadi nafasi ya nne inayoshikiliwa na JKT Tanzania iliyocheza mechi 17 na kukusanya pointi 28.
Kwa sasa Singida Black Stars iliyocheza mechi 15, imekusanya pointi 25, wakati Pamba Jiji iliyopo nafasi ya tano na pointi 25, imecheza mechi 16.
Kwa mujibu wa ratiba ilivyo, vinara Yanga katika mwezi Aprili, inatarajiwa kucheza mechi tano za ligi kabla ya kukutana na Simba, Mei 3 mwaka huu ikiwa ni baada ya duru la kwanza kumalizika bila ya kufungana. Safari hii Simba itakuwa mwenyeji.
Katika mechi tano za ligi mwezi Aprili, Yanga itaanzia nyumbani Aprili 4 kucheza dhidi ya Tanzania Prisons, kisha Aprili 8 itaifuata Pamba Jiji na Aprili 16 itarejea nyumbani kuikaribisha Mbeya City.
Mechi hizo tatu, Yanga itacheza bila ya kipa wake namba moja, Djigui Diarra aliyepewa adhabu ya kusimamishwa mechi tatu kwa utovu wa nidhamu.
Baada ya hapo, itakuwa mgeni wa KMC (Aprili 19) na kumalizia nyumbani dhidi ya Coastal Union (Aprili 30).
KMC (nafasi ya 16), Tanzania Prisons (nafasi ya 15), Mbeya City (nafasi ya 14) na Coastal Union (nafasi ya 13), ndiyo wapinzani wa Yanga katika mechi za mwezi Aprili waliopo kule chini wakipambana kuondoka kwenye hatari ya kushuka daraja, wakati Pamba Jiji (nafasi ya 5), ikihitaji kupambana kulinda rekodi ya kutopoteza mechi ya nyumbani msimu huu baada ya kuwa ya pili nyuma ya Yanga kwa kukusanya pointi nyingi nyumbani msimu huu.
Pamba Jiji nyumbani msimu huu imekusanya pointi 19 katika mechi tisa, wakati Yanga inazo 22 katika mechi nane.
Ukija kwa Simba, mechi za Aprili ina Mzizima Dabi dhidi ya Azam itakayochezwa Aprili 5 ambapo itakuwa ugenini, kabla ya hapo, Aprili 2, 2026, itaikaribisha Coastal Union.
Kwa mwezi Aprili, Simba itacheza mechi sita ambazo ikikamilisha kabla ya kukutana na Yanga, zitalingana michezo, hivyo kuchanga kwao karata vizuri kutawafanya kuingia Dabi ya Kariakoo wakiwa juu ya Yanga au karibu zaidi na kuufanya mchezo huo kuamua nafasi ya kwanza.
Hivi sasa, Yanga imeiacha Simba pointi saba ambapo pia zimetofautiana michezo miwili. Endapo timu hizo kila moja ikishinda mechi zake za Aprili, basi zitakapokutana Mei 3, tofauti ya pointi itakuwa moja pekee ambapo Yanga itakuwa juu ya Simba.
Mechi zingine za Simba kwa mwezi Aprili ni dhidi ya Fountain Gate (Aprili 9, ugenini), Namungo (Aprili 15, ugenini), JKT Tanzania (Aprili 19, nyumbani) na Tanzania Prisons (Aprili 29, nyumbani).
Azam na Singida Black Stars ambazo msimu uliopita zilimaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo, nazo mwezi Aprili zina mechi za kimkakati ikiwamo moja inayozikutanisha zenyewe.
Mechi hiyo itapigwa Aprili Mosi, siku ambayo ligi itaendelea, huku Singida Black Stars ikiwa mwenyeji. Kumbuka mechi ya duru la kwanza zilishindwa kufungana.
Mechi zingine za Singida Black Stars kwa mwezi Aprili ni dhidi ya TRA United (Aprili 5, ugenini), KMC (Aprili 8, nyumbani), Mashujaa (Aprili 16, ugenini), Pamba Jiji (Aprili 20, nyumbani) na Mtibwa Sugar (Aprili 30, nyumbani).
Kati ya mechi hizo sita, Singida itacheza nyumbani mara nne, huku mbili ikienda ugenini, huku rekodi ya nyumbani msimu huu ikiacha maswali mengi kwani tayari imefungwa dhidi ya Yanga na Simba mfululizo.
Kwa Azam ukiondoa zile mbili zinazofuata dhidi ya Singida Black Stars (Aprili 1, ugenini) na Simba (Aprili 5, nyumbani), zingine ni dhidi ya Mbeya City (Aprili 9, ugenini), JKT Tanzania (Aprili 16, nyumbani), Namungo (Aprili 20, nyumbani), TRA United (Aprili 30, ugenini). Jumla kwa mwezi Aprili ni mechi sita kama ilivyo kwa Singida Black Stars na Simba. Yanga pekee ndiyo itacheza mechi tano.
Kati ya timu ambazo zipo karibu zaidi kushuka daraja ni KMC yenye pointi nane, ikiachwa tano na inayofuatia Tanzania Prisons na Mbeya City zenye pointi 13 kila moja, huku Coastal Union ikiwa nazo 15.
Timu hizi zinapambana kutoka kule chini, lakini KMC ndiyo yenye mtihani zaidi kwani mechi 16 zilizopita, imekusanya nane ambapo wastani wake ni kwamba kila baada ya mechi mbili ndiyo inakusanya pointi moja.
Katika mwezi Aprili, KMC ikiteleza kidogo tu, pengine ikashuka daraja mapema zaidi huku ratiba ikionyesha itacheza mechi tano dhidi ya Mbeya City (Aprili 3, ugenini), Singida Black Stars (Aprili 8, ugenini), Tanzania Prisons (Aprili 14, nyumbani), Yanga (Aprili 19, nyumbani) na Fountain Gate (Aprili 28, nyumbani).
Katika ratiba hiyo, KMC itacheza na timu mbili zinazopambana zote kutoka chini ambazo ni Tanzania Prisons na Mbeya City, pia timu mbili zinazopambana kule juu, Yanga na Singida Black Stars, lakini pia dhidi ya Fountain Gate ambayo nayo haipo mbali na mstari wa kushuka daraja, hivi sasa ni ya 12 kwa tofauti ya pointi moja na timu iliyopo katika kucheza mtoano.
Kocha wa KMC, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, anasema mechi tano zijazo za Ligi Kuu Bara kwa kikosi hicho zitakuwa za uamuzi mgumu wa hatima yao.
“Kadri unavyozidi kupoteza ndivyo ambavyo pia morali ya wachezaji inapungua, tumekuwa na muda mzuri wa kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika mechi zetu zilizopita, ili turudi imara na kutoka sehemu tuliyopo,” anasema Baresi.
Tangu mara ya mwisho Februari 22, 2026 KMC ifungwe mabao 2-0 dhidi ya Azam, haijacheza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara huku ikiwa na mapumziko ya takribani mwezi mmoja na siku sita ya kujiimarisha zaidi.
