Geita. Baadhi ya wananchi katika mgodi wa Msasa uliopo kata ya Runzewe,wilayani Bukombe,wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu tukio la kutitia kwa maduara kadhaa katika mgodi huo ambapo baadhi wameeleza juu ya uwepo wa majeruhi na vifo.
Tukio hilo lilitokea Jana Jumapili Machi 29,2026, ambapo asubuhi zilianza kusambaa taarifa katika mitandao ya kijamii zikieleza miongoni mwa waliofariki ni pamoja na wafanyakazi, wachuuzi mbalimbali waliokuwa na biashara, wanawake wanaosaga mawe (wapiga ukware) waliokuwa juu ya maduara 10.
“Hizo taarifa zinaweza zikatolewa zingine ambazo haziaminiki ila kweli jana walikuwa wamekusanyika watu wengi wakiwamo wauza maji, wapiga ukware na wachimbaji, maana palititia na baadhi ya watu wakaenda chini muda huo nilikuwa napita karibu na eneo hilo,”amesema mchimbaji aliyejitambulisha kwa jina moja la Emma.
Shuhuda huyo ameeleza kushangazwa na taarifa ya Polisi inayoeleza kutokuwepo kwa vifo wala majeruhi, akibainisha kuwa watu waliumia.
Shuhuda mwingine ambaye hakutaka kutaja jina anayeishi Runzewe, alieleza kuwa gari la kusafirisha wagonjwa, lilikuwa likienda mgodini na kurudi kituo cha afya Uyovu ingawa hawana hakika ikiwa lilikuwa likileta majeruhi au kuchukua vifaa vya uokozi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, inadaiwa idadi kubwa ya watu waliokuwa juu ya maduara hayo na wengine waliokuwa chini ya ardhi wakichimba, wanadhaniwa kufariki dunia kutokana na kuangukiwa na kifusi, huku baadhi wakidai mabomu ya machozi kutumika kuwatawanya wachimbaji waliotaka kusaidia uokozi na kuomba ufanyike uchunguzi wa kina.
Baada ya uvumi huo, Jeshi la Polisi jana saa 2 usiku, lilitoa taarifa ya kanusho juu ya uwepo wa vifo. Taarifa hiyo ilieleza kuwa kilichotokea ni kutitia kwa maduara yaliyokuwa yamefungwa baada ya taarifa za wasimamizi kubaini uwepo wa dalili mbaya za kiusalama.
Ikifafanua zaidi taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, ilieleza kuwa tukio la maduara manne ya uchimbaji madini katika mgodi wa dhahabu wa Msasa, uliopo Runzewe magharibi,Wilaya ya Bukombe,mkoani Geita, saa 4:00 asubuhi wakati wa ukaguzi wa kawaida uliokuwa ukifanywa, mmoja wa wakaguzi alibaini kibanda kilichokuwa karibu na maduara hayo kimeanza kutitia, alitoa tahadhari kwa wenzake waliokuwa katika eneo hilo na wote walifanikiwa kutoka nje salama.
Alifafanua kuwa maduara hayo hayakuwa katika shughuli za uzalishaji kwani tayari yalikuwa yamefungwa.
“Hatua za haraka za kiusalama zimechukuliwa kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na idara na mamlaka nyingine za Serikali kwa ushirikiano na wananchi. Tathmini ya awali imebaini kuwa hakuna mtu aliyekuwa ndani ya maduara hayo wakati wa tukio, hivyo hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokea.”
Kwa sasa eneo hilo lina ulinzi mkali hakuna mwananchi anayeruhusiwa kulisogelea.
