Unguja. Ukosefu wa mitaji, majukumu ya malezi yasiyolipwa, ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni miongoni mwa changamoto ambazo zinawakumba wanawake wengi na kurejesha uchumi wao nyuma.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (OCGS), mwaka 2025 yaliripotiwa matukio 1,228, mwaka 2024 yalikuwa matukio 1,809 na mwaka 2023 yalikuwa matukio yalikuwa matukio 1,954.
Kuwapo kwa matukio haya licha ya idadi yake kuendelea kupungua mwaka hadi mwaka, kunatajwa kumnyima mwanamke kupata usawa wa kujishughulisha katika shughuli za uzalishaji mali.
Hata hivyo, katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa kushiriki shughuli za kukuza uchumi na kujiinua kimaendeleo, Serikali zote mbili kwa kushirikiana na wadau zimekuwa zikiweka mikakati mbalimbali mwanamke anaondolewa vikwazo na kumnyanyua na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo.
Hilo linajidhihirisha kufuatia kuanzishwa mradi wa kukuza usawa wa kijinsia Tanzania (Pamoja) unaolenga kuwaunganisha wanawake na fursa za kiuchumi amba
Baadhi ya wanawake kisiwani hapa wanaeleza vikwazo hivyo lakini wanavyopambana kuondokana navyo huku wakiendelea kupata vipato na wengine kuendesha familia zao na namna mpango huo utakavyozidi kuwaimarisha kiuchumi.
Zurima Hamad ni mmoja wa wajasiriamali kisiwani hapa anakiri namna wanawake wanavyokumbana na changamoto hizo ambazo pia zinachagizwa zaidi na tamaduni na mila, kwani mwanamke anachukuliwa kama mlezi wa familia.
“Mtazamo hasi ndio unatuumiza wanawake, wakati mwingine usipopambana unaweza ukajikuta huwezi kufanya chochote kwa sababu sisi tunaonekana wakukaa nyumbani, lakini kupitia mradi huu tumeshajipanga namna ambavyo wanawake wataongezewa ujasiri kufanya mambo makubwa,” anasema
Hata hivyo, Hadija Msellem anasema wanawake wana mchango mkubwa na kwa sasa wameanza kuvikimbia vikwazo kutokana na jitihada mbalimbali za uhamasishaji wanawake kushiriki shughuli za kiuchumi na kupata vipato badala ya kutegemea wanaume.
Anasema ujio wa mradi huo utaongeza wigo kwa kundi hilo kupata uelewa na kuondolewa vikwazo ikiwa ni nia za kupambana na vikwazo vya kiuchumi.
Katika mradi huu ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) jumla ya wanawake na watoto 41,000 watanufaika katika kipindi cha miaka mitano.
Mpango huo unatilia mkazo jamii, hasa wanawake, kwa kuwapa fursa za kiuchumi na kubadilisha mitazamo ya kijamii kuwaona wanawake kama pambo la nyumbani na hawana nafasi kushiriki uzalishaji mali kwa ajili ya vipato vyao na taifa kwa ujumla.
Mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB) Tanya Dilima amesema walianza mjadala huu kwa tathmini ya jinsia na tathmini ya pato la Taifa mwaka 2022, na hiyo iliunda msingi wa uchambuzi kuona umuhimu wa kuwapo na uwezeshaji kwa wanawake ili kuwaondolea vikwazo vya kiuchumi.
Anasema Zanzibar, kama sehemu nyingine nyingi za dunia, wanawake wanafanya shughuli za kiuchumi, na wana uthabiti mkubwa, lakini wanakabiliwa na vikwazo.
“Upatikanaji mdogo wa fedha, majukumu ya malezi yasiyolipwa, na kukabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia. Kwa hivyo ‘Pamoja’ inakusudiwa kujibu moja kwa moja hali hizo zote. Na kupitia mradi huu, Zanzibar sio tu kuwekeza katika fursa za kiuchumi kwa wanawake, lakini pia kuimarisha mifumo inayounga mkono usalama wao,” anasema Dilima.
Kundi hilo pamoja na mambo mengine, litawezeshwa kwa kupatiwa elimu na mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa biashara kabla ya kuanza kupatiwa mikopo.
Katibu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambaye ameteuliwa kuwa balozi nchini Saudi Arabia, Balozi Zena Said anasema Serikali inatambua masuala ya ukatili na udhalilishaji yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya nchi na tayari imeanza kutayarisha bajeti kwa kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia.
Kwa mujibu wa Zena, mwanamke ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kuhimili mambo makubwa tofauti na inavyodhaniwa na watu wengi.
“Nguvu itaongezeka katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji hasa kwa kina mama na watoto kwa kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa huduma kwa waathirika wa udhalilishaji,” anasema.
Katika kukabiliana na changamoto za msongo wa mawazo na afya ya akili, mradi huu unalenga pia kutoa huduma za kisaikolojia kwa waathirika wote wa vitendo vya udhalilishaji pamoja na wanajamii kwa ujumla kupitia kituo kitakachojengwa mahususi kwa shughuli hizo.
Kituo hicho kitatoa huduma za ushauri nasaha ambazo zinasaidia kuwarudisha katika hali zao za kawaida na kuimarisha ustawi wao huku vituo vya malezi ya kutwa vitajengwa na baadhi ya majengo kukarabatiwa katika kuhakikisha suala la mama anashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na mtoto akilelewa katika mazingira salama.
“Utaakisi dhana ya kuhakikisha haki na usawa wa mwanamke unafikiwa kwa mustakabali wa jamii kwa ujumla,” anasema Balozi Zena.
Anasema hawatakiwi kushughulikia tu ukatili baada ya kutokea, bali pia kuangalie jinsi ya kuuzuia usitokee, kubadilisha mitazamo katika jamii na kuunganisha nguvu kuwa na jamii bora na imara zaidi.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdallah anasema katika kuleta ufanisi mbali na mambo mengine mradi huo utashughulikia kukuza fursa za kiuchumi kwa wanawake kupitia mifumo ya fursa za kijamii kwa kuimarisha vikundi vyao vya uzalishaji.
Anasema mradi huo ambao unatekelezwa kwa miaka mitano, utawezesha wanawake kiujuzi na kifedha ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
“Vikundi vya wanawake vitapatiwa mafunzo ya ujasiriamali, uongozi, usimamizi wa biashara pamoja na mbinu za kutafuta masoko ya bidhaa wanazozalisha,” anasema Abeida
Baada ya mafunzo hayo vikundi vitapata fursa ya kuomba mikopo kati ya Sh500,000 hadi Sh30 milioni kulingana na aina na ukubwa wa biashara, ambapo watakuwa na muda wa kurejesha mkopo huo kati ya miezi 12 hadi 24. Mikopo hiyo itasimamiwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), ambapo jumla ya Sh33 bilioni zitatumika katika utekelezaji wake.
Utekelezaji wake utaendana na mpango mkuu wa kitaifa wa kupambana na Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa Awamu ya pili (NIPA-VAWC ll 2025-2030) zikiwa ni jitihada za kitaifa kutokomeza vitendo vya udhalilishaji.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul anasema utekelezaji wa mradi huo ni ahadi ya kufanya kazi pamoja, kuthamini uimara wa Zanzibar na kuleta fursa zaidi zitakazofika katika maeneo ya utekelezaji mradi na kubadilisha maisha ya wananchi.
“Tuchukue fursa hii ili kuhakikisha manufaa ya matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni chachu muhimu katika ujasiriamali na uwekezaji wenye kuzingatia kuinua maisha ya wanawake.”
Kwa upande wake Rashid Abbas Ali anasema wanawake wanaweza kufanya mambo makubwa iwapo wakishikwa mkono na kupewa msukumo kutoka kwa watu wa karibu badala ya kuwakatisha tamaa na kuwatolea maneno ya kejeli.