****
Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekabidhi mashine mbili za kisasa za kutoa joto kwa watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni iliyopo Kata ya Mwabepande, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema msaada huo ni mwendelezo wa taasisi hiyo kushiriki katika shughuli za kijamii sambamba na jukumu lake la kupambana na rushwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila.
Amesema TAKUKURU imeona umuhimu wa kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kutokana na uhitaji wao wa uangalizi maalum, huku akibainisha kuwa mashine hizo zitasaidia kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi.
“Tunatambua bado kuna changamoto ya vifo vya watoto wachanga, hususan njiti, hivyo tunaona ni wajibu wetu kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha huduma zinaboreshwa na maisha ya watoto yanaokolewa,” amesema Chalamila.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo akieleza kuwa umekuja wakati muafaka kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za watoto wachanga katika hospitali hiyo.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Makala Neja, amesema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa vifaa tiba, hususan katika kuwahudumia watoto njiti wanaohitaji uangalizi wa karibu.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa mashine hizo utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kusaidia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa watoto wachanga.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni, Dk. Zena Abdu Suleiman, amesema mashine hizo zitasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma za watoto njiti na kuongeza nafasi yao ya kuishi.
Aidha, ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo na kuwataka wadau wengine kuendelea kujitokeza kusaidia sekta ya afya ili kuboresha huduma kwa makundi yenye uhitaji mkubwa, hususan mama na mtoto.





.jpg)









