Tanzania yashauriwa kuchangamkia fursa dunia ikiyumba kiuchumi

Dar es Salaam. Wakati mvutano wa kisiasa hasa Mashariki ya Kati ukiendelea kubadilisha mifumo ya biashara, soko la nishati na mwelekeo wa uwekezaji wa mitaji. Imeelezwa kwamba Tanzania bado itaendelea kuwa eneo lenye kuaminika kwa uwekezaji wa muda mrefu iwapo itachukua hatua mbalimbali ili isiathirike na machafuko hayo kiuchumi.

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki katika mjadala ulioandaliwa na ALN Tanzania (A&K Tanzania) kwa kushirikiana na Bankable, ambapo viongozi waandamizi kutoka sekta za benki, viwanda na nishati walijadili namna mabadiliko ya kimataifa yanavyoathiri uamuzi wa uwekezaji duniani na maana yake kwa nafasi ya ushindani ya Tanzania.

Ukiwa na kauli mbiu isemayo: “Dunia inayobadilika, faida ya ushindani wa Tanzania”, wadau walibainisha Tanzania bado ni eneo linalovutia kwa uwekezaji.

Licha ya mazingira ya uwekezaji kuwa magumu hivi sasa katika nchi nyingi, upatikanaji wa fedha umepungua, na wawekezaji wanazingatia zaidi usalama wa mitaji yao katika nchi wanazowekeza.

“Mitaji bado ipo, lakini vigezo vimebadilika. Sasa swali sio tu kama fursa za biashara bado zipo, bali kama zinaweza kutekelezwa kwa wakati kutokana na hali ilivyo hivi sasa,” alisema Ed Williams, Mkurugenzi wa ALN Tanzania.

Mjadala huo ulifanyika huku misukosuko ya kimataifa katika Mashariki ya Kati ikiendelea, ambayo imesababisha ongezeko la bei ya mafuta kwa takriban asilimia 20 na kuvuruga njia muhimu za usafirishaji.

Kwa Afrika Mashariki, hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na kutokuwa na uhakika katika minyororo ya ugavi. Hata hivyo, wazungumzaji walisisitiza misukosuko hii pia inachochea mabadiliko mapana ya kimataifa ambayo yanaweza kuipa Tanzania fursa.

Minyororo ya ugavi inapungua, uwekezaji wa mitaji unatishiwa na hali iliyopo ambapo wawekezaji wanatafuta masoko tulivu yenye nafasi nzuri ya kikanda.

Uwepo wa hali ya utulivu katika Bahari ya Hindi hapa nchini, miundombinu inayoboreshwa, rasilimali asilia na utulivu wa kisiasa vinaipa nafasi nzuri Tanzania kunufaika na mabadiliko ya biashara na uwekezaji.

Manzi Rwegasira, Mtendaji Mkuu wa Stanbic Bank Tanzania, alibainisha ingawa hali ya sasa inaathiri moja kwa moja bei za bidhaa, pia inaonesha umuhimu wa uwepo wa masoko thabiti na imara.

Vilevile, Mohamed Mohamed, Mtendaji Mkuu wa kampuni ya kimataifa ya Tanzania ya kuhifadhi mafuta (Tiper), alisema miundombinu ya usafirishaji ikiwemo bandari na uwezo wa kuhifadhi bidhaa za mafuta inakuwa kigezo muhimu cha ushindani kadiri minyororo ya ugavi ya kimataifa inavyobadilika.

Kwa upande wake, Vineet Verma, Meneja Mkuu wa Kioo Limited, alisema wazalishaji wanazidi kutathmini maeneo ya kupanua uzalishaji kwa kuzingatia si gharama pekee, bali pia uhakika wa nishati, usafirishaji na upatikanaji wa masoko ya kikanda maeneo ambayo Tanzania inaendelea kufanya vizuri.

Wazungumzaji walikubaliana kuwa fursa ya Tanzania haitokani tu na rasilimali zake, bali pia na jinsi inavyoweza kuzitumia kwa ufanisi katika mazingira magumu ya kimataifa.

“Misukosuko ya kimataifa imefungua dirisha la fursa kwa masoko kama Tanzania. Tuna msingi mzuri eneo, rasilimali na utulivu lakini kitakachotutofautisha ni uthabiti wa utekelezaji na namna tunavyojiweka kama mshirika wa kuaminika wa muda mrefu kwa wawekezaji na mitaji,” alisema Shemane Amin, Mshirika wa ALN Tanzania.

Akiwasilisha andiko lake, Atiq Anjarwalla, Mshirika Mwandamizi wa ALN (Falme za Kiarabu), alihimiza Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki kutumia kwa mkakati rasilimali zao za asili ili kuimarisha uchumi na kujilinda dhidi ya athari za migogoro ya Mashariki ya Kati.

Alisisitiza hali ya sasa ya kimataifa inaleta changamoto pamoja na fursa, na kuzitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuimarisha masoko yao na kuongeza ustahimilivu wa kiuchumi.

“Mfumuko wa bei utaongezeka, na gharama ya maisha itapanda kwa kiasi kikubwa, bila hatua madhubuti, tunaweza hata kushuhudia kupungua kwa shughuli za usafiri kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta.”

Akihitimisha, Chris Green, Mkurugenzi wa ALN Tanzania, alisema matukio ya hivi karibuni Mashariki ya Kati yameongeza hali ya kutotabirika katika masoko ya kimataifa, na kutoa wito kwa Tanzania kuchukua hatua madhubuti kulinda nafasi yake ya kikanda katika biashara.