Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesema ameshindwa kufanya ukaguzi wa hesabu kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa mwaka wa fedha 2024/25 kutokana na mashauri yanayoendelea.
Mbali na chama hicho, Kichere amesema amefanya ukaguzi katika vyama vingine na kwamba Chama cha Wananchi (CUF) na NRA vimepata hati zenye mashaka, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo upungufu wa nyaraka toshelevu zinazothibitisha uhalali wa malipo.
CAG ameeleza hayo leo, Jumatatu Machi 30, 2026 aliposoma muhtasari wa ripoti yake ya ukaguzi inayoanzia Juni 2024 hadi Julai mwaka 2025, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ameeleza hakuweza kufanya ukaguzi wa hesabu wa Chadema kwa mwaka wa fedha 2024/25 baada ya kupata taarifa kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu mashauri yanayoendelea mahakamani.
Aidha, amesema vyama vya siasa vya CUF na NRA vimepata hati zenye mashaka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo upungufu wa nyaraka toshelevu zinazothibitisha uhalali wa malipo.
Hata hivyo, Kichere amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 amefanya kaguzi 1,553 zikihusisha 1,339 za hesabu za fedha, 18 za ufanisi, mifumo ya Tehama 137 na kaguzi maalumu na za kiuchunguzi 47.
Katika kaguzi hizo, amesema ametoa jumla ya hati 1,339 ukilinganisha na hati 1,301 alizotoa katika mwaka wa fedha 2023/24.
Ameeleza hati 221 zinahusu tawala za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, 225 zinahusu mashirika ya umma, 562 Serikali kuu na 331 miradi ya maendeleo.
Kati ya hati hizo, amesema zinazoridhisha ni 1,326 sawa na asilimia 99, zenye shaka 10 na mbaya ni moja, huku taasisi mbili akishindwa kutoa maoni ya ukaguzi.
Amezitaja taasisi zenye hati zenye mashaka ni Bodi ya Korosho, Bodi ya Chai, Kiwanda cha dawa cha Keko, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kyela-Kasumuru ameshindwa kutoa maoni.
Amesema Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kondoa, Handeni zimepata hati zenye mashaka, huku Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) ikipata hati mbaya.
Hati nyingine zenye mashaka, amesema zimekwenda kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na Msalala.
