Serikali kuanziasha Ligi ya wazawa tu, Makonda ataja sababu

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda amefichua mpango wa kuanzishwa kwa Ligi ya Soka ambayo itahusisha wachezaji wazawa tu.

Makonda amesema hayo juzi wakati akifungua kikao cha Maofisa Michezo na Utamaduni kinachofanyika jijini Arusha.

“Namshukuru sana Mheshimwa Waziri Mkuu, Dokta Lameck Mwigulu na juzi nimefanya naye kikao ameridhia kuyaandikia mashirika yote nchini yawe na timu.

“Mmeona juzi timu ya TRA (United) inavyofanya vizuri. Sina maana ya kutoka droo. Lakini tunatamani kuona Bandari wanafufua timu yao. Shirika letu la ndege watakuwa na timu yao. Shirika letu la reli watakuwa na timu. Tunataka tuone mpaka TANAPA, tunataka tuone Ngorongoro.

“Sasa hizi timu itakuwa bora sana nyinyi maofisa michezo mkachochea vijana wengi wanaotoka kwenye maeneo yenu wawe kwenye hizi timu kuliko hizi timu kuajiri watu wanaotoka nje. Na ndio maana tunatamani kuanzisha ligi ya ndani ambayo wachezaji wanaocheza ni wa ndani tu na haya ndio maelekezo.

“Kwamba tuanzishe ligi pia ambazo watacheza wazawa ili kuwatengeneza na kuwapandisha waweze kufika hatua ya kuwa nao wakubwa,” amesema Makonda.

Makonda amesema kuwa lengo la uwepo wa ligi hiyo ni kusaidia kutoa fursa kwa idadi kubwa ya wachezaji wazawa ambayo wamekuwa hawaipati katika Ligi Kuu ya NBC.

Kanuni ya Ligi Kuu Tanzania Bara 2025/2026 inalazimisha kila klabu kuwa na wachezaji wasiozidi 12 wa kigeni.

“Klabu ya Ligi Kuu inaruhusiwa kusajili wachezaji kumi na wawili (12) wa kigeni kutoka sehemu yoyote duniani (mazingatio kwa kanuni ya 62:4 ya kanuni hizi),” inafafanua kanuni ya 62(1) ya Ligi Kuu msimu huu.