Pemba. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi anatarajiwa kuzindua mbio za Mwenge za Uhuru 2026, katika Uwanja wa Mchezo Gombani, Pemba Aprili 2, 2026.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu, Machi 30, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana wa, Joel Nanauka na Waziri wa Vijana na Ajira Zanzibar,Shaaban Ali Othman walipozungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar.
Nanauka amesema Mwenge ni Tunu ambayo imejikita katika kukuza misingi ya Taifa imara kama kuzingatia maadili uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika maendeleo endelevu nchini.
Picha tofauti za vijana wa alaiki wakifanya mazoezi katika uwanja wa Gombani Pemba ikiwa ni maandalizi ya ufunguzi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa unaotarajiwa kuzinduliwa uwanjani hapo Aprili 2 mwaka huu
Wiziri huyo amesema maandalizi ya uzindizi wa mbio hizo yamekamilika na baada ya uzinduzi utazunguka mikoa yote 31 ya Tanzania (Bara na Zanzibar) ambako mawe ya msingi yatawekwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo huku mingine ikizinduliwa.
Amesema tangu Mwenge wa Uhuru kuasisiwa na Rais wa awamu ya ya Kwanza Tanzania, Mwalim Julius Nyerere, falsafa yake imekuwa ni kuleta umoja na mshikamano na kujenga misingi imara ya uwajibikaji.
Amesema Mwenge wa Uhuru umekuwa na dhamira ya kupambana vitendo viovu kama rushwa na dawa za kulevya ambavyo vinakwaza maendeleo ya taifa.
Amesema Mwenge wa Uhuru ulioasisiwa mwaka 1961 ulioungwa mkono ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, pale waliposisitiza wananchi kumiliki njia kuu za uchumi na kuimarisha huduma za kijamii na umiliki wa ardhi.
Amesema hatua hiyo imeleta umoja na upendo na wananchi kuwa na uhuru wa kuendeleza harakati za kijamii katika kujitafutia maisha bila ya ubaguzi wowote.
Amesema Aprili 26, 1964 mbio za Mwenge wa Uhuru zilianza rasmi nchini ikiwa ajenda kuu ni kulinda uhuru wa nchi, matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano.
Awali, Waziri wa Vijana na Ajira Zanzibar, Shaaban Ali Othman amewataka wananchi na makundi yote ya vijana nchi kuhakikisha wanajitokeza katika kushiriki uzinduzi huo.
Amesema vijana wapaswa Zaidi kushiriki kwa kuwa Serikali imekuwa ikiweka mkazo kuwaangalia wao kwa karibu na kuwawezesha.
Amesema wizara itaendelea kuyafikia makundi tofauti na kuyapa uwelewa juu ya umuhimu wa Mwenge wa Uhuru tangu kuanzishwa kwake.
Picha tofauti za vijana wa alaiki wakifanya mazoezi katika uwanja wa Gombani Pemba ikiwa ni maandalizi ya ufunguzi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa unaotarajiwa kuzinduliwa uwanjani hapo Aprili 2 mwaka huu
“Nawaombeni vijana mjitokeze kushiriki katika uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru ukiwa ujembe: Tanzania ni yetu sote tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo,” amesema Shaaban.
Kilele cha mbio za Mwenge wa uhuru kama ilivyo kawaida kitakuwa Oktoba 14, 2026 mkoani Rukwa, ikiwa pia ni kumbukumbu ya miaka 27 ya kifo cha Mwalimu Nyerere na kilele cha wiki ya vijana.
